Aliyekua kiungo na nahodha wa klabu ya Liverpool, Steven George Gerrard ameonyesha kuchukizwa na tabia zinazoonyeshwa na mshambuliaji wa klabu hiyo, Raheem Sterling ambaye anadaiwa kuwa katika shinikizo la kutaka kuondoka Anfield.

Gerrard, ambaye tayari ameshaelekea nchini Marekani kujiunga na klabu ya Los Angles Galaxy, amesema Stering hapaswi kufanya upuuzi aliouonyesha katika jamii ya wapenda mchezo wa soka duniani.

Amesema mshambuliaji huyo anatakiwa kufahamu heshima aliyojiwekea katika klabu ya Liverpool, na katu hapaswi kuivunja na mwishowe kuonekana sio mtu katika watu.

Kiungo huyo aliyeitumikia Liverpool kwa zaidi ya miaka 20, amethibitisha kuzungumza na Sterling na kumueleza ukweli wa mambo kuhusu suala la nidhamu, huku akimsisitizia kuwa na utamaduni wa kujiheshimu baada ya kuheshimiwa.

Gerrard, amemtaka mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 19, kuwa muwazi na kutosita kusema chochote mbele ya meneja wa klabu ya Liverpool, Brendan Rodger na si kuanza kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu.
Siku mbili zilizopita Sterling, alidaiwa kukacha mazoezi ya Liverpool kwa kuonyesha ishara ya kushinikiza suala lake la uhamisho lipewe kipaumbele kwanza, baada ya klabu ya Man City kuonyesha dhamira ya kweli ya kutaka kumsajili kwa zaidi ya paund million 40.

Jambo lingine ambalo limeonekana kama ukosefu wa adabu kwa mshambuliaji huyo, ni taarifa zilizochapishwa kama tetesi hapo jana ambapo zilieleza atakuwa tayari kubaki Liverpool, endapo meneja Bredan Rodgers ataonyeshwa mlango wa kutokea (kufukuzwa).

Hata hivyo tetesi hizo zilikanushwa na wakala wa Sterling kwa kusema si za kweli na amevishutumu vyombo vya habari kwa kutaka kumuharibia mteja wake katika kipindi hiki ambacho kimekaa kimtego kwa ajili ya kutengeneza ama kuharibu maisha.

Mo Farah Arudisha Majibu Kwa Vitendo
Serena Ajiwekea Rekodi Wimbledon Championship