Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali imetekeleza miradi mingi ya huduma za jamii kila eneo hivyo watendaji wa Halmashauri zote nchini wanatakiwa waendelee kubuni miradi mikubwa na kuitekeleza kwa kutumia fedha za makusanyo ya ndani, badala ya kutegemea fedha kutoka Serikali kuu pekee.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumza na watumishi, madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya Songwe akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa mkoani Songwe na kusema watendaji wahakikishe miradi inasimamiwa kikamilifu na kukamilika kwa wakati.
Amesema, “Katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan tumejifunza mambo mengi ikiwemo miradi mingi ya halmashauri kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu. Watendaji wote wa halmashauri lazima wapanue wigo wa ukusanyaji mapato.”
Aidha, Majaliwa pia ametumia fursa hiyo kuwataka watumishi wa umma waondoe urasimu katika kuwahudumia wananchi na badala yake wafanye kazi kwa weledi, uaminifu na uadilifu ili waweze kuongeza tija katika utekelezaji wa majukumu yao.