Aliyekua nahodha na mshambuliaji wa klabu ya Arsenal, Thierry Daniel Henry, amewatahadharisha wachezaji wa klabu hiyo, kuelekea katika mchezo wa hii leo ambapo The Gunners watawakaribisha mabingwa wa soka kutoka nchini Ujerumani, FC Bayern Munich.

Henry, ambaye kwa sasa amerejea kaskazini mwa jijini London na kukabidhiwa timu ya vijana ya Arsenal, amewasihi wachezaji wa Arsene Wenger kuwa tayari kwa mpambano wa leo lakini kubwa aliloliainisha ni hatari ya mshambuliaji kutoka nchini Poland, Robert Lewandowski.

Amesema, Lewandowski atakua mwiba mkali kwa safu ya ulinzi ya Arsenal, endapo itashindwa kuwa makini wakati wote, kufuatia ujanja na ujasiri wa uchezaji wa mshambuliaji huyo ambao umeonekana kwa siku za hivi karibuni.

Amesema, mshambuliaji huyo anapaswa kutazamwa kwa jicho la tatu ili asiweze kuleta madhara makubwa kwa Arsenal, hivyo ni jukumu la kikosi kizima cha The Gunners kuhimizana, kitakapokua uwanjani kwa dakika 90.

Hata hivyo Henry, amesisitiza ushindi kwa kikosi cha klabu yake ya Arsenal ili kurejesha matumaini ya kusonga mbele kwenye michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya, baada ya mambo kuwa mabaya katika michezo miwiwli ya mwanzo ya kundi la sita.

Arsenal walikubali kufungwa na Dynamo Zagreb mabao mawili kwa moja katika mchezo wa kwanza wa kundi la sita na kisha wakapoteza mchezo wa pili dhidi ya mabingwa wa soka kutoka nchini Ugiriki Olimpiakos, kwa kufungwa mabao matatu kwa mawili.

Robert Lewandowski ameshafunga mabao 22, katika michezo 16 aliyocheza tangu mwanzoni mwa msimu huu, ikijumuisha ile ya timu yake ya taifa ya Poland, ambayo ilikua ikiwania nafasi ya kufuzu kucheza fainali za mataifa ya barani Ulaya.

SDL Yapigwa Kalenda
Ratiba Ya Mzunguuko Wa 11 Yapanguliwa