Napenda kumpongeza tena Rais Mstaafu, Dk. Jakaya Kikwete kwa kutazamwa na kukubalika na Umoja wa Afrika kuwa ndiye kiongozi anayefaa kwa sasa kuongoza ujumbe maalum wa kusaidia kuzima ‘moto’ mkubwa wa mgogoro unaoendelea nchini Libya.

Uteuzi wa Dk. Kikwete ulitangazwa Januari 31 mwaka huu katika mkutano wa viongozi wa juu wa mataifa ya Afrika uliofanyika jijini Addis Ababa nchini Ethiopia, akichukua nafasi ya Mohamed Dileita wa Djibouti, aliyefanya kazi hiyo tangu mwaka 2014.

Mgogoro wa Libya ni mkubwa, ambapo kumekuwa na Serikali mbili hivi sasa nchini humo, ile iliyopiga kambi Mjini Tripoli ikiwa ni wale waliokuwa wanajeshi watiifu wa Muammar Gaddafi na wale wa jiji la Tobruk. Mgogoro huo uliogeuka kuwa vita ulizaliwa baada ya kuondolewa kwa nguvu madarakani na kuuawa kwa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Muammar Gaddafi.

Hata hivyo, Dk. Kikwete na jopo lake wakifanikiwa haitakuwa mara ya kwanza kwa Dk. Kikwete kwani mwaka 2007/2008 alifanikiwa kuuzima ‘moto’ wa vurugu mbaya kuwahi kutokea nchini Kenya, za baada ya uchaguzi mkuu wa nchi hiyo zilizosababisha mauaji na watu kukosa makazi.

Viongozi wengi walienda nchini Kenya lakini hakukuwa na matumaini. Lakini ujumbe wa Dk. Kikwete ulizaa matunda ambapo siku chache baada ya kufanya mazungumzo na  Mwai Kibaki na Raila Odinga, mahasimu hao wa kisiasa walikubaliana kuunda serikali ya umoja wa kitaifa.

Kwa kumbukumbu hizo, ni dhahiri kuwa Rais huyo mstaafu amejaliwa hekima na Baraka za kuzima moto wa kisiasa na kuwa mpatanishi kadiri awezavyo, na kweli Mungu huambatana naye kwenye tendo hilo jema. Kwa waamini wa dini ya Kikristo tunaweza kumuita mwenye heri kwani imeandikwa ‘Heri wapatanishi maana hao wataitwa wana wa Mungu’.

Hata hivyo, ni vyema kumkumbusha kuwa wakati anajitahidi kuzima moto wa jirani kwa hekima na busara alizojaliwa, asizisahau cheche za moto zilizoanza kuonekana hapa nyumbani kupitia mgogoro wa uchaguzi wa Zanzibar.

Anashauriwa kufumbia macho lawama anazotupiwa ambazo tayari amezikanusha, zinazodai kuwa yeye ndiye aliyeagiza kufutwa kwa matokeo ya uchaguzi wa Zanzibar alipokuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano na Mwenyekiti wa CCM. Huu sio muda wa lawama, ni muda wa kuokoa jahazi.

Dk. Kikwete bado ana nafasi kubwa ya kusaidia katika kuziweka mezani pande mbili zinazovutana za CUF na CCM, [bila kujali kuwa yeye ndiye mwenyekiti wa CCM].

Kwa bahati nzuri mgogoro huu anaufahamu vizuri kwani umeanza wakati wa utawala wake, hivyo bado ni mtu muhimu sana wa kuzima cheche zinazoonekana visiwani humo.

Utakuwa sio uungwana kukumbuka juhudu alizoanza kuzionesha wakati akiwa Rais wa kukutana na Maalim Seif (CUF) na kufanya naye mazungumzo ingawa matunda ya mazungumzo hayo hayakuonekana dhahiri.

Ninaamini sio lazima uwe Rais wa Tanzania ndio uwe na uwezo wa kutatua mgogoro wa Zanzibar kama ambavyo hivi sasa wengi wameelekeza nguvu zao kumshawishi Rais John Magufuli wakidai ndiye pekee anayeweza kumaliza mzozo huo.

Tukumbuke Dk. Kikwete anaenda Libya kama mjumbe na sio Rais, huenda akafanikiwa. Naamini anaweza pia kufanya hivyo Zanzibar, japo changamoto ni kofia ya Uenyekiti inayomfanya aonekane yuko upande fulani.

Mafunzo FC Yawafuata AS Vita
Watoto walishtaki mahakamani kanisa la TB Joshua