Hotuba ya Rais John Magufuli katika sherehe za Kuukaribisha mwaka mpya wa kimahakama imezua zogo hususan ahadi yake ya shilingi bilioni 250 kwa mahakama ili ikamilishe kusikiliza kesi za ukwepaji kodi zenye thamani ya shilingi trilioni 1.

Rais Magufuli aliahidi kuwa fedha hiyo ikipatikana, ataipa kada hiyo kiasi cha shilingi bilioni 250 na shilingi bilioni 750 zitatumika kununua ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Baadhi ya wadau walioikosoa sehemu ya hotuba hiyo ni wakili maarufu wa kujitegemea, Peter Kibatala ambaye amedai kuwa ahadi hiyo ya rais kwa Mahakama ilikuwa na sura inayoweza kupelekea mahakama kutoa hukumu zake huku ikikumbuka ahadi ya fedha zilizotolewa na serikali.

Alisema kesi hizo ambazo serikali ndiyo inayoshitaki zinaweza kupelekea mahakama kutotenda haki huku akitoa mfano kuwa mahakama ni kama imetekwa na ahadi hiyo.

“Hii ni sawa na na mtu amteke nyara mtoto wako na akuahidi kuwa ili umpate lazima utoe milioni tano,” alisema Kibatala.

“Kwa muktadha wa kauli ya Rais, Mahakama imetekwa, kama Rais anasema Serikali inatarajia kupata Shilingi trilioni moja katika kesi hizo na fedha hizo zitakapopatikana Mahakama ipatiwe Shilingi Bilioni 250, kuna maanisha hapa lazima Serikali ishinde kesi ili Mahakama inufaike, hapa kweli kutakuwa na haki? alihoji Wakili huyo.

Maoni hayo ya Kibatala ambaye pia ni Mkurugenzi wa Sheria na Haki za Binadamu wa Chadema, yaliendana na maoni ya Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe.

Zitto alieleza kuwa pamoja na kwamba hotuba hiyo imependwa na baadhi, lakini kulikuwa na mapungufu kwa kuwa mahakama haipaswi kufanya kazi kwa uoga au upendeleo. Alihoji itakuaje kama Jaji Mkuu na Majaji wengine wakihukumu kesi hizo za trilioni 1 ndani ya siku chache kwa matakwa ya serikali huku ikiziwaza shilinigi bilioni 250 iliyoahidiwa.

Hata hivyo, Rais wa Chama Cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Flaviana Charles aliunga mkono hotuba ya Rais na kueleza kuwa alikuwa akijibu changamoto alizoelezwa na kada hiyo ya mahakama.

“Mahakama itabaki kama chombo huru cha kusimamia haki ya sheria za nchi,: alisema Flaviana.

Naye wakili wa Mahakama Kuu, Silvanus Mayenga alisema kuwa pamoja na ahadi ya Rais, bado taratibu za kimahakama lazima zitafuatwa na kwamba ucheleweshwaji wa kesi hautokani tu na fedha.

“Kuna msitari kati ya alichokisema Rais Magufuli katika kutekeleza kazi za Mahakama, na  uhalisia wa taratibu za mahakama katika kuendesha kesi zake ambao unazingatia sheria,” alisema Mayenga.

Baba yake Rihanna ampigia Chapuo Chris Brown kwa mwanae
Mifuko ya Jamii yabanwa koo