Taarifa zinasema kuwa jina la kiungo mchezeshaji kutoka nchini Kenya, Francis Kahata, limeingia kwenye rada za Azam FC katika usajili wa msimu ujao.

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu tetesi zizagae zikidai kuwa Simba SC wapo kwenye mchakato wa kuachana na kiungo huyo mwenye rasta baada ya mkataba wake kumalizika.

Taarifa zinaeleza kuwa, jina la kiungo huyo linatajwa kuwepo kwenye orodha ya wachezaji wanaowaniwa na timu hiyo katika msimu ujao.

“Azam wamekuwa hawana kiungo mchezeshaji mwenye uwezo wa kuchezesha na kutuliza mashambulizi wakati timu inapozidiwa zaidi ya Sure Boy (Salum Aboubakary).

“Hivyo hivi sasa wapo katika mipango ya kumsajili Kahata kwa ajili ya kuiimarisha safu yao ya kiungo katika kuelekea msimu ujao.

“Na kingine wanachotaka kumsajili Kahata ni kwa ajili ya michuano ya kimataifa ambayo wana uhakika nayo watashiriki mwakani, hivyo kwa uzoefu wake ataisaidia timu hiyo,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Mkuu wa Maudhui ya Simba, Ally Shanty kuzungumzia hilo alisema hana taarifa za Kahata kwani hayupo na timu hivi sasa tangu timu ilipotolewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Kama unavyofahamu Kahata alisajiliwa kwa ajili ya michuano ya kimataifa na siyo Ligi Kuu Bara, hivyo hayupo na timu kwa hivi sasa,” alisema Shantry.

Kwa upande wa Ofisa Habari wa Azam, Thabiti

Zakaria amesema: “Masuala ya usajili yote yapo chini ya kocha ambaye yeye ndiye anajua asajili mchezaji gani, hivyo hilo suala halijafika mezani kwangu na kama mchezaji akisajiliwa basi ni lazima tutamtangaza, hivyo tusubiri.”

Aweso aagiza aliyeidhinisha mradi wa maji yenye chumvi kuondolewa kazini
Sabaya, walinzi wake walivyopandishwa kizimbani leo