Kamati ya Kudumu ya Bunge inayosimamia Masuala ya UKIMWI, Kifua Kikuu, Dawa za Kulevya na Magonjwa yasiyoambukiza imeridhishwa na utekelezaji wa mradi wa Timiza Malengo unaotekelezwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), unaolenga kuwawezesha vijana kiuchumi.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dkt. Alice Kaijage ameyasema hayo wakati wa ziara ya Kamati ya kukagua utekelezaji wa mradi huo katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara mkoani Morogoro ambapo amesema kuanzishwa kwa mradi kumewafanya vijana kuamka kifikra na kuamini wana uwezo wa kujieletea maendeleo.
Amesema, “Katika Halmashauri ya Ifakara tumekuta serikali na watendaji wanafanya kazi kwa bidii sana tumewaona vijana wana ujasiri, wamefungua miradi, biashara, wengine wanafuga kuku, nguruwe na kufungua magenge ni kwa sababu serikali kupitia watendaji imewawezesha vijana hawa na imewasaidia kuepuka vishawishi mbalimbali.”
Aidha, amewataka vijana hao kusimamia malengo yao kwa kutumia vyema fedha walizopewa ili kuanisha miradi hatua itakayosaidia kuepuka vishawishi vitakavyosababisha kupata maambukizi ya virusi vya UKIMWI kutokan an ahali duni ya Maisha.
Ameongeza kuwa, “Afua mojawapo katika kutekeleza na kupambana na masuala ya UKIMWI ni afua ya ulielimishaji rika ambayo inahusika kukinga na kuelimisha wasichana rika balehe ili wajiamini na kupambana na maisha yao wenyewe pamoja na kuepuka vishawishi,”Alieleza Makamu Mwenyekiti huyo.”
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu , Ofisi ya Waziri Mkuu , Sera, Bunge na Uratibu, Kaspar Mmuya amesema afua za UKIMWI hazitekelezwi na wizara moja pekee bali zinatekelezwa na wizara zote za kisekta na wadau wa ndani na nje ya Nchi .
Amesema, “Malengo ya Serikali katika kupambana na UKIMWI imejielekeza ifikapo mwaka 2030 kusiwe na maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI na pasiwepo na mtu yeyote mwenye virusi vya UKIMWI ambaye atakufa kwa ugonjwa huo pamoja na kuondoa unyanyapaa ifikapo mwaka 2030.”
Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko amesema tume hiyo inashirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia katika mtaala wa uelimishaji rika ambao unafundishwa kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika Halmashauri 18.
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero mkoani Morogoro, Hanji Godigodi akiongea katika eneo hilo ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuunga mkono juhudi za taasisi za serikali na binafsi zinazopambana kudhibiti maambukizi ya virusi vya UKIMWI huku akiwataka watendaji kusimamia fedha za mradi ili kutimiza malengo ya kuanzishwa kwake.
Awali, mmoja wa wanufaika wa mradi huo Bi. Gladness Champunga aliishukuru serikali na TACAIDS kwa kuanzisha mradi akisema umemnufaisha kama kijana kujipatia kipato kupitia saluni yake ambapo inamuwezesha kukidhi mahitaji muhimu.
Mradi huo unatekelezwa ikiwa ni Awamu ya pili kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2023 katika Halmashauri za Wilaya 18 zilizopo katika Mikoa mitano ya Dodoma, Geita, Morogoro, Singida na Tanga ukihusisha vijana wanaotoka katika kaya masikini.