Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa imewashukia baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya ikisema wanatumia vibaya mamlaka waliyopewa kwa kuamrisha watumishi wa umma kuwekwa ndani kwa makosa yasiyostahili adhabu hiyo.
Akisoma taarifa ya shughuli za kamati hiyo kwa mwaka 2016/17, mjumbe wa kamati Ester Mahawe amesema, ipo mifano kadhaa ikiwa ni pamoja na mkuu wa mkoa mmoja nchini aliamuru daktari wa mkoa wake awekwe  rumande kwa sababu hakutangaza kuwapo kwa ugonjwa wa kipindupindu.”
Bila kutaja majina, ametoa mfano mwingine wa mkuu wa wilaya moja ya Mkoa wa Dar es Salaam aliyeamuru watumishi waliochelewa kazini wawekwe ndani na mwingine wa Mkoa wa Arusha aliyeamuru mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni nchini awekwe ndani kwa kuandika habari kuhusu kero ya ukosefu wa maji, ambayo mkuu huyo wa wilaya alitafsiri kuwa ni uchochezi.
Mahawe ametoa mfano mwingine kuwa ni mkurugenzi wa halmashauri aliyeamuru mwalimu wa sekondari kudeki darasa mbele ya wanafunzi kwa sababu ni chafu.
“Mkuu wa mkoa kutumia lugha zisizofaa kwa watumishi kuwa ni wezi, wajinga wasiokuwa na akili timamu, hawa ndio vichaa tunaohangaika nao ni kudhalilisha utu wa mtu na kuvunja misingi ya Katiba,” amesema Mahawe.
Aidha,ametoa ufafanuzi huku  akisema Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 sura ya 97 imeweka masharti muhimu kwa mkuu wa mkoa na wilaya ikiwa atahitaji kutumia mamlaka ya kuamrisha mtu akamatwe.
Hata hivyo amewataka viongozi wote na wabunge kuzingatia sheria, kanuni, miongozo na utaratibu uliopo na kwamba, kinyume na hapo watakuwa wameshindwa kutimiza wajibu wa kuwa mfano kwa wanaowaongoza.
Mbali na kamati, wabunge waliochangia mjadala wa taarifa hiyo wamesema mambo yanayofanyika ni matumizi mabaya ya madaraka ya mamlaka waliyopewa.

Magazeti ya Tanzania leo Februari 4, 2017
Video: Taarifa ya jeshi la polisi kuhusu watuhumiwa wa uhalifu Dar