Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amesema kuwa kitendo cha serikali kuzuia ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuchapishwa ni kutokana na kigezo cha taifa kupewa mikopo kwa riba kubwa.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amebainisha kuwa kuzuiwa kwa ripoti hiyo kutazorotesha mahusiano ya taifa na shirika hilo na kudai kuwa wakati wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete hakukuwepo na zuio lolote.
“Wakati wa Kikwete aliendeleza mahusiano mazuri na IMF japo watu walikuwa wanamsema kuwa ni mzee wa kutembea nchi za nje lakini IMF waliweza kuja kufanya mkutano mkubwa hapa kwetu mwaka 2009,” amesema Prof. Lipumba.
Aidha, amesema kuwa katika utawala wa awamu ya tano kumekuwa hakuna programu yoyote ya Shirika la Kimataifa, programu ya mwisho ilikuwa mwaka 2014 na wakati huo wanaojadili bajeti bungeni ni vizuri ripoti ya uchambuzi wa IMF ichapishwe ili wabunge wapate kuisoma na kujua kama sera zinakidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi wa nchi.
Kwa upande wake Waziri wa Fedha, Dkt. Philip Mpango amesema kuwa serikali haijazuia ripoti ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ila wanaendelea na mazungumzo na shirika hilo.