Mchakato wa Uchaguzi Mkuu unaendelea huku presha ikiongezeka katika majimbo mengi, mvutano katika jimbo la Nyamagana jijini Mwanza umemalizika usiku wa manane ambapo Stanslaus Mabula (CCM) ametangazwa kuwa mbunge mpya wa jimbo hilo akimshinda Ezekiel Wenje (Chadema).

Mvutano huo umekamilika huku Ezekiel Wenje akikataa kusaini fomu ya matokeo kwa madai kuwa hakutendewa haki kwani baadhi ya kura hazikuwa na mihuri pamoja na dosari nyingine. Hivyo, CCM wamefanikiwa kurudisha majimbo yote mawili ya Mwanza Mjini yaliyokuwa yakishikiliwa na Chadema.

Katika hatua nyingine, matokeo ya jimbo la Ubungo yameendelea kusubiriwa kwa hamu, huku mgombea ubunge kwa tiketi ya Chadema, Saed Kubenea amelalamikia ucheleweshwaji wa matokeo katika jimbo hilo huku akidai kuwa matokeo hayo yanacheleweshwa makusudi.

Kubenea ambaye alikuwa akisubiri matokeo usiku kucha katika chumba cha kufanyia majumuisho huku mshindani wake Dk.  Didas Masaburi wa CCM akidaiwa kutohudhuria zoezi hilo, amedai kuwa matokeo aliyoyajumuisha kwenye vituo vyote yanampa ushindi wa kishindo.

“Kwa matokeo yaliyopo kwenye vituo vya kata, yanaonesha kwamba mimi au sisi nikiwa na maana na chama changu, tumeweza kushinda kwa zaidi ya asilimia 75. Na katika kata nane za jimbo la Ubungo, mimi nimeongoza kata zote na na nimefanikiwa kupata madiwani 7 kati ya 8,” alisema Kubenea.

Wafuasi wa vyama vyote wanasubiri kwa hamu matokeo ya ubunge wa jimbo hilo ambalo kabla ya kugawanywa, lilikuwa likishikiliwa na John Mnyika wa Chadema ambaye hivi sasa amehamia katika jimbo la Kibamba.

 

CUF Wajibu Baada Ya CCM Kudai Wamehujumiwa Uchaguzi Zanzibar
Halima Mdee Afunguka Baada Ya Taarifa Kusambaa Kuwa Ameshindwa Mapema