Mchezo wa ufunguzi wa michuano ya Copa America Centenario kati ya Marekani dhidi ya Colombia umemalizika kwa Colombia kuanza vyema michuano hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Colombia walianza kufungua akaunti ya mabao kwa bao la mapema kwenye dakika ya 8 kupitia kwa Cristian Zapata baada ya mlinzi wa Marekani anayekipiga na Milan, Cameron kushindwa kumkaba Eric Carderon aliyeachia mkwaju wa chini uliyemkuta mfungaji.

Ndoto za Marekani kutaka kukomboa bao hilo ziliendelea kufifia baada ya Colombia kuandika bao la pili kwenye dakika ya 42 kwa njia ya mkwaju wa penalti iliyofungwa na James Rodriguez baada ya mlinzi wa Marekani kuunawa mpira katika eneo la hatari.

Kipindi cha kwanza kilimalizika kwa Colombia kuibuka kifuambele kwa mabao hayo 2-0, kipindi cha pili kilianza polepole kulinganisha na kile cha kwanza lakini licha ya Colombia kuzidiwa umiliki wa mpira haikuwasaidia Marekani kupata walau bao la kufutia machozi.

David Ospina aliisaidia timu yake kutofungwa bao la tatu kwenye dakika ya 64 baada ya kufanya kazi nzuri ya kupangua mkwaju ulioelekezwa kwenye lango lake.

Licha ya kufanya mabadiliko ya hapa na pale, Marekani haikuweza kubadili matokeo hayo na mpira kumalizika kwa Colombia kuibuka na pointi tatu muhimu.

Kwa matokeo hayo, Colombia inakalia usukani wa Kundi A ikiwa na pointi tatu na mabao 2 huku USA ikoshikilia mkia wa kundi hilo.

Uchaguzi Wa Young Africans: Manji Na Wenzake Wavuka Hatua Ya Kwanza
Mbwana Samatta Awapa Nafasi Young Africans Dhidi Ya TP Mazembe