Matokeo ya uchaguzi wa CCM uliomuwezesha Dkt. John Magufuli kuwa mgombea wa kiti cha urais kwa tiketi ya chama hicho yameendelea kuzua sintofahamu kwa timu ya Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa iliyomtaka akihame chama hicho.

Rafiki mkubwa wa Lowassa, mbunge wa zamani wa jimbo la Monduli, Luteni Lepilal Ole Molloimet ni mmoja kati ya waliojitokeza hadharani kumshawishi akihame chama hicho na kujiunga na kambi ya upinzani.

“Tena mimi nataka a-cross. Afanye hivyo, aende Ukawa kwa sababu ni yeye pekee ndiye mwenye uwezo wa kulisaidia taifa hili,” Molloimet aliiambia Raia Tanzania.

Alisema Dkt Magufuli anaweza kuliongoza taifa hili lakini hana uwezo wa kupambana na Ukawa tofauti na Lowassa aliyekuzwa katika maadili ya Kimasai, mvumilivu na mwenye uwezo wa kukemea.

Mzee Molloimet ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya mbalimbali nchini alizungumzumzia taarifa za kutiliwa shaka kwa maadili ya Lowassa na kudai kuwa mfumo mzima wa chama hicho kwa sasa unanuka rushwa.

“Mfumo mzima ndani ya CCM kwa sasa unanuka rushwa, Magufuli hatafanya chochote kama chama kiko namna hii. Maadili ndani ya CCM yanakiukwa, takriban asilimai 80 ya wana CCM ni walafi hawawajali masikini wala usalama wao. Kwa wao ni matumbo yao tu,” gazeti hilo linamkariri.

Jana kulikuwa na taarifa za uhakika za Edward Lowassa kuitisha mkutano na waandishi wa habari nyumbani kwake Masaki, Dar es Salaam lakini mkutano huo hicho kiliahirishwa ghafla bila sababu yoyote kutolewa.

Kuarishwa kwa kikao hicho kulizua tetesi nyingi ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa taarifa kuwa alitaka kuzungumzia mambo mazito ya chama hicho pamoja na mustakabari wake kisiasa.

Taarifa ambazo hazikuthibitishwa zilidai kuwa timu ya Lowassa ilikuwa na mazungumzo ya siri na viongozi wa Chadema kuhusu uwezekano wa kuhamia katika chama hicho cha upinzani. Lakini taarifa hizo zilikanushwa na viongozi wa ngazi za juu wa Chadema.

“Hizi habari ndio kwanza nazisikia kwako. Hatujawahi kuzungumzia na sioni namna gani huyu bwana naweza kujiunga na Chadema,” alisema Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Profesa Abdallah Safari.

Abakwa Mara Ya Pili Baada Ya Polisi Kumtumia Kama Mtego Kuwakamata Wabakaji
Picha: Mrembo Wa Miaka 26 Ashinda Taji La Miss USA 2015