Rais John Magufuli amemsimamisha Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli Tanzania (RAHCO), Mhandisi Benhard Tito baada ya kubainika kuhusika katika ukiukwaji mkubwa wa taratibu za Manunuzi katika utoaji wa zabuni ya ujenzi wa reli ya Kati kwa kiwango cha kisasa.

Mhandisi Benhadard Tito (katikati)

Mhandisi Benhadard Tito (katikati)

Akizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue alisema kuwa ripoti ya ukaguzi uliofanywa na Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma (PPRA) ilibaini kuwa Mhandisi Tito na Bodi ya RAHCO walihusika katika kuvunja sheria ya manunuzi ya umma katika mchakato wa utoaji wa zabuni ya ujenzi huo.

Alisema rais Magufuli ameivunja Bodi ya RAHCO baada ya ukaguzi wa PPRA kubaini ukiukwaji wa taratibu za utoaji zabuni, Bodi hiyo haikuchukua hatua stahiki bali ilionekana kutetea kilichofanyika.

Aidha, Balozi Sefue alisema kuwa rais Magufuli ameagiza PPRA kufanya uchunguzi na kuchukua hatua dhidi ya kampuni za kandarasi zilizopewa zabuni za ujenzi wa reli hiyo ya kati katika kiwango cha kisasa.

Alisema kuwa Rais Magufuli amemtaka Mhandisi Tito kushirikiana na mamlaka husika zitakazofanya uchunguzi wa kina kuhusu utoaji wa zabuni hiyo.

Katika hatua nyingine, Balozi Sefue alisema kuwa Rais Magufuli ameivunja Bodi ya Mamlaka ya Reli Tanzania (TRL) kufuatia kutoridhishwa na namna ambavyo ilishughulikia ripoti ya manunuzi ya mabehewa ya treni, iliyobaini ukiukwaji mkubwa wa taratibu za manunuzi na ubadhirifu.

 

Rais Apiga Marufuku Safari za Ndege Daraja la Kwanza kwa Watumishi wa Umma
Mbunge afariki ghafla kwenye kikao cha bunge