Mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli amesema kuwa endapo atachaguliwa kuwa rais wa Tanzania, serikali yake itaewezesha tafiti mbalimbali zitakazosaidia katika kukuza uchumi nchini.

Magufuli ameyasema hayo jana alipohutubia maelfu ya wananchi katika jimbo la Misungwi mkoani Mwanza.

“Tutasaidia kuwezesha utafiti wa masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na utafiti kwenye kilimo chetu na hapa Ukiligulu ili tuweze kujiinua kiuchumi,” alisema Dkt. Magufuli.

Magufuli Misungwi

Aliongeza kuwa serikali yake itafufua viwanda vya pamba vilivyodorora na kujenga viwanda vipya vya kutengeneza nguo ili watanzania waweze kukombolewa na uchumi wa viwanda. Alisema anashangazwa kuona pamba inayolimwa Misungwi inapelekwa Ulaya kisha watanzania wanarudishiwa nguo zilizovaliwa kwa muda na watu wa Ulaya (mitumba) waliotumia pamba hiyo, na kwamba hali hiyo itakoma baada ya kufufua na kujenga viwanda nchini.

Aliongeza kuwa serikali yake itaboresha maisha ya wafanyakazi wote ikiwa ni pamoja na kupunguza makato ya kodi kwenye mishahara yao.

“Kwa ndugu zangu wafanyakazi nataka mtuamini kwamba tunataka kuboresha mishahara ya wafanyakazi pamoja na kujenga nyumba za walimu,” alisema.

Alisema kuwa serikali yake itahakikisha inapunguza asilimia ya makato ya kodi kwenye mishahara ya wafanyakazi kutoka asilimia zaidi ya 11 iliyopo hivi sasa.

 

Lowassa Aimba Wimbo Mmoja na Mbowe Mbeya
Magufuli Alivyoitikisa Mwanza, Ahadi Ya Kuigeuza ’Geveva’