Bila shaka unamkumbuka Joseph Kibwetere, yeye ni raia wa Uganda na alikuwa ni Mwalimu wa shule ya msingi na mara kadhaa alijiingiza katika harakati za siasa lakini akashindwa kuwashawishi wananchi na kuuteka umma kwa sera zenye mashiko, hivyo akatafakari njia nyingine ya kutoka akaona DINI itamlipa.
Kupitia kona hiyo, gari la Kibwetere likawaka na huko akawapumbaza watu kwa kujiita ‘Nabii na Mtume’. akawateka kwa maneno matamu na yenye ushawishi huku akitumia vibaya vifungu vya maandiko MATAKATIFU.
Kwa kujiamini, aliwaahidi waumini wake kuwapeleka peponi, lakini mwisho wao ukawa mbaya kwani aliwauwa kwa kumwaga petroli na kuwachoma moto akiwaaminisha kwamba mwisho wa dunia umefika.
Tukio hili ni baya kuwahi kutokea Barani Afrika, kwani aliwapa watu imani iliyojaa udanganyifu na kuacha majonzi makubwa huku yeye ikidaiwa kuwa alijificha na baadaye kutoroka.
Joseph Kibwetere. Picha ya Facebook.
Tukio mfanano.
Kutoka nchini Uganda, sasa uzao mfanano na wa Kibwetere umeibuka kwa ghafla nchini Kenya, Mchungaji anayefahamika kwa jina la Paul Mackenzie akimiliki Kanisa la Good News International, lililopo mji wa Malindi amesababisha huzuni majonzi na vilio kwa familia athirika na wananchi.
Ikatolewa ripoti ya watu wanne kufariki baada ya kushawishiwa kufunga kula na kunywa hadi wafe, ili waweze kukutana na MUNGU huku wengine 11 wakiwahishwa Hospitali ya Kaunti ya Pwani ya Kilifi nchini Kenya wakiwa dhohofu hali.
Polisi ikasema watu watatu kati ya hao 11 waliokua wakipokea matibabu, walikuwa katika hali mbaya kiafya huku wakiendelea kupata matibabu na wanane wakiwa katika hali nzuri baada ya kutibiwa.
Tukio hili likaacha tafakari kubwa kwa jamii, lakini wakati wakitafuta majibu Idara ya upelelezi DCI eneo la Malindi ikasema imeanza uchunguzi, baada ya kupata habari kuwa bado kuna watu zaidi katika msitu mmoja eneo la Shakahola, lilipo shamba la mhubiri huyo ambapo na watu wengine 15 wakapatikana wakiwa mahututi.
Paul Mackenzie wa Kanisa la Good News International. Picha ya Tuko News.
Kilichofuata ni Mchungaji huyu kutafutwa, akatiwa nguvuni na baadaye akashitakiwa kwa madai ya kuwataka waumini wake kufa njaa, ili wafike mbinguni kwa kasi, akapewa dhamana na baadaye
Mahakama ikamuondolea dhamana.
Shughuli ya kukagua shamba la Mchungaji Mackenzie lenye ukubwa wa ekari 800 lililotumika kuweka kambi ya watu hao ikaendelea, Wapelelezi wakaona muinukoi wa tuta mfano wa kaburim wakafukua, hapo miili mitatu ya Mama na watoto wawili igagundulika siku ya kwanza ikaisha.
Zoezi likaingia siku ya pili, ya tatu na ya nne miili ya watu kumi ikapatikana ikiwa imezikwa maeneo tofauti, pia mtu mmoja akapatikana akiwa amechoka na yupo hoi kwa mfungo huo akisubiri kufa akakutane na MUNGU kwa haraka na akawahishwa Hospitali kuokoa maisha yake.
Miongoni mwa miili iliyofukuliwa siku hiyo ilikuwa ni ya familia ya watu watano, yaani baba, mama na wanawawe watatu, ambao wote walikua wamezikwa sehemu moja, …. inasikitisha …. inaumiza.
Baadhi ya watu waliokolewa kwenye tukio hilo. Picha ya The Star.
Mpaka sasa miili 21 ya Waumini wa Kanisa hilo la Good News International Church imegundulika, baada ya maafisa hao wa Ofisi ya DCI kuchimba makaburi mafupi yaliyokuwa kwenye ardhi hiyo ya Mackenzie iliyopo Kijiji cha Shakahola Kaunti ya Kilifi.
Kiongozi huyu wa Kanisa, Paul Mackenzie anawauwa kwa kuwalazimisha Waumini wake kuanzia Watoto wadogo hadi Watu wazima kufunga kula na kunywa ili wafe kama njia ya moja kwa moja ya kufika kwa Muumba wao.
Rejelea muhimu.
Wakati fulani, Mzee wetu na Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete alipata kusema katika moja ya hotuba zake kuwa, “akili za kuambiwa changanya na za kwako,” lakini pia hata katika maandiko upande wa Biblia ukisoma Hosea 4:6 unasema Watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa; kwa kuwa wewe umeyakataa maarifa, mimi nami nitakukataa wewe.
Miili iliyokutwa shambani kwa Mchungaji Paul Mackenzie. Picha ya Radio Jambo.
Eti Mchungaji Mackenzie, ambaye kwa sasa yuko Mahabusu huku uchunguzi dhidi yake ukiendelea, naye anadaiwa ameweka mgomo wa kula akisimamia anachokiamini na Polisi wanaema bado makaburi mengine yenye kina kirefu hayajachimbwa.
Historia yake kimatukio.
Mara kadhaa, amewahi kukamatwa na vyombo vya dola, ilikuwa ni mwaka 2019 alipohojiwa kuhusu elimu aliyokuwa akitoa kwa waumini kutozingatia elimu na kudai kuwa elimu ni dhambi na Machi mwaka huu wa 2023, kuhusiana na vifo vya watoto lakini mara zote, aliachiliwa kwa dhamana na kesi zote mbili bado zinaendelea mahakamani.
Sasa Wanasiasa wa eneo hilo, wameitaka mahakama kutomwachilia huru wakati huu wakikemea kuenea kwa madhehebu katika eneo la Malindi, huku wengi wakistaajabia, wakihuzunika na wakiitaka Serikali kuzimulika taasisi za kidini kwa kina ambazo nyingi zimekuwa zikikumbwa na kashfa za ulaghau na kuwapotosha watu.
Paul Mackenzie anadaiwa amegoma kula akiwa mahabusu. Picha ya The Star.
Kuhusu Good News International Ministries.
Mackenzie anasema kanisa hili alilianzisha Agosti 17, 2003 na akaweka matawi katika mikoa mbalimbali nchini Kenya ikiwemo (Nairobi, Watamu, Malindi, Kitale, Machakos, Naivasha, Mombasa, Mwea, Lunga Lunga, Matano manne) na Makao Makuu yake yapo katika eneo la Malindi Furunzi.
Anasema, dhamira ya huduma za Kanisa lake ni kuwalea waamini kwa ukamilifu katika masuala yote ya kiroho ya Kikristo wakati wakijiandaa kwa ujio wa pili wa Yesu Kristo kupitia mafundisho na uinjilisti huku akihubiri unabii juu ya nyakati za mwisho.
Kisa cha kusisimua na kuhuzunisha.
Wengi wameingia katika mtego huu, na kibaya zaidi huaminishwa mambo ambayo maamuzi yake wakati mwingine hutafakarisha zaidi, kwa mfano aliyekuwa mfanyakazi wa shirika moja la Ndege la Qatar yeye ni miongozi mwa watu waliofariki akiwa na mwanaye wa kiume ambao walidanganywa na mtumishi huyu kuwa watakutana na Yesu.
Anafahamika kwa jina la Betty aliyekuwa nafasi ya uhudumu ndani ya ndege na inaarifiwa kuwa aliacha kazi miaka 11 iliyopita, akiuza ardhi yake kwa Shilingi milioni 7 za kenya na pesa zote akampatia kiongozi huyu wa ibada nabii Paul Mackenzie.
Baadaye anakubali ‘mfungo wa kifo’ na kibaya zaidi ni kuwachukua na mtoto wake Jason, naye akafa akiwa amefunga sambamba na babu yake aliyekuwa akienda kufanya kazi naye katika shirika hilo la Qatar, ambapo Betty alirejea Kenya kwa mazishi lakini alitoweka muda mfupi baadaye.
Betty (picha ndogo kushoto) wakati akihudumu shirika la ndege na kulia akiwa na Mwanaye Jason.
Dada yake wa Nairobi anadai Betty alimwachia mumewe barua kabla ya kuondoka, akidokeza kwamba huenda asirudi tena na aliuza vitu vyake vyote, akawachukua watoto wake, na kuelekea Malindi baada ya kusikia kutoka kwa rafiki yake kwamba wote wangekutana na Yesu Aprili 8, 2023 ambapo hakuonekana tena akiwa hai, bali mwili wake na watoto.
Baadhi ya waokoaji katika zoezi hilo, wanadai eti kulikuwa na kikundi maalumu kilichosimamia mauaji hayo na kuzika watu wanaokufa kwa mfungo, ikiwa ataonekana mtu kashtukia zoezi hilo na anataka kukimbia basi atakamatwa na kufungwa kamba kisha wanamalizia na kumzika.
Lakini kabla ya kuingia eneo hilo ni lazima simu na mali zako vyote unakabidhi kwa kiongozi wa kiroho na inasemekana wengi wa waliofariki ni watoto wadogo maana Nabii huyo (Mackenzie), alitangaza kwamba watoto ndio watangulizwe kwanza na kupewa kipaumbele cha kwenda kukutana na Yesu. INASIKITISHA.
Paul Mackenzie (kulia), macho yako yanakushitaki na damu iliyopotea inakulilia.
Paul Makenzie, unayejiita Nabii na Mtumishi wa Mungu nini kimekusbu mpaka ukawapeleka waumini wako kwenye ardhi ya shamba lako, akawaambia wafunge kula na kunywa mpaka watakapokufa, ili wakutane na MUNGU wao bila kuwafafanulia azma yako na yao baada ya kufa? ama kweli ukistaajabu ya Musa utayaona ya Firauni.
Mchungaji Anthony Lusekelo, al-maarufu kama ‘Mzee wa Upako’ aliwahi kusema, “wewe unaamini nini? Baki na imani yako, lakini usivunje sheria za nchi.” TAFAKARI msemo huo huku ukiomba MUNGU akupe uwezo wa kutambua baya na jema.
Imeandaliwa na Humphrey Edward.