Timu ya Taifa ya Marekani imekuwa timu ya kwanza kuwasili nchini Qatar, huku timu nyingine shiriki 31 zikitarajia kuwasili nchini baadae juma hili na juma lijalo.

Marekani imewasili usiku wa kuamkia leo Ijumaa (Novemba 11) katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Doha ikiwa zimebaki siku chache kabla ya kuanza kwa michuano ya Kombe la FIFA la Dunia 2022.

Marekani imepangwa Kundi B katika michuano ya mwaka huu pamoja na Timu za Mataifa ya England, Wales na Iran.

Taifa hilo litaanza kampeni ya kusaka Ubingwa wa Dunia Novemba 21 kwa kucheza dhidi ya Wales katika Uwanja wa Ahmad bin Ali mjini Al Rayyan.

Novemba 25 Marekani itacheza mchezo wake wa Pili dhidi ya England katika UWanja wa Al Bayt, mjini Al Khor na kisha itamaliza na Iran Novemba 29 katika Uwanja wa Al Thumama mjini Doha.

Fainali za Kombe la Dunia zinatarajiwa kuanza kutimua vumbi Novemba 20, 2022 na kufikia kilele Desemba 18, 2022.

Biden kukutana faragha na Xi Jinping
Kocha Walid Regragui ajilipua kwa Hakim Ziyec