Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi Taifa, James Mbatia amevuliwa uanachama wa chama hicho, kufuatia maamuzi ya Mkutano mkuu wa chama na kumvua cheoa Makamu Mwenyekiti wake, Angelina Rutairwa huku viongozi wote waliohusika na ubadhilifu wa mali akiwemo Mbatia wakitakiwa kuchukuliwa hatua.

Mkutano huo, wa Septemba 24, 2022 unaofanyika jijini Dodoma umefikia hatua hiyo baada ya Kaimu Mwenyekiti wa chama hicho, Haji Ambari Hassan kutaja tuhuma saba mbele ya wajumbe 224 kati ya 368 waliopo kwa mujibu wa Katiba ya NCCR – Mageuzi, zinazomkabili Mbatia na mbili zikimkabili Bi. Rutairwa.

Mbatia anakabiliwa na tuhuma za kuuza mali za chama, ikiwemo mashamba na nyumba katika maeneo mbalimbali, ambapo Hassan akiwaambia wajumbe kuwa viongozi hao walipelekewa hati ya wito na tuhuma na walitakiwa kujibu ndani ya siku 14 kama katiba inavyoelekeza lakini hawakujibu na hawakufika ili kujitetea.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi Taifa, James Mbatia.

“Tuliwapelekea mwaliko na hata ile hati hawakuijibu na hawajafika kuja kujitetea mbele ya wajumbe kama katiba inavyotaka na badala yake walikimbilia mahakamani kuzuia kwa mara nyingine mkutano huo,” amefafanua Kaimu huyo Mwenyekiti wa Chama cha NCCR – Mageuzi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini la NCCR – Mageuzi, Joseph Selasini amesema halmashauri kuu ya chama hicho imewavua uanachama watu 10 kwa utovu wa nidhamu, akiwemo Edward Simbeye na mkutano huo unafanyika ili kujadili mambo mbalimbali ikiwemo suala la mpasuko ndani ya chama.

Mapema hivi karibuni, Msajili wa vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alishauri kwenda mahakamani, kwani ratiba ya mkutano huo ilimfikia kabla ya kufunguliwa kwa kesi hiyo na tayari NCCR-Mageuzi, upande wa Mbatia imefungua kesi ikiwemo ya kuomba kusimamishwa kwa mkutano huo.

Wanne wa familia moja wauawa, 15 mbaroni
Wakimbizi nchi ya tatu waanza maisha mapya Ughaibuni