Beki wa kati tegemeo wa Simba, Mzimbabwe Method Mwanjali sasa yu tayari kuanza mazoezi na wenzake baada ya kupata nafuu ya maumivu ya goti.

Mwanjali hakuwemo kwenye kikosi kilichokwenda Dodoma na Arusha kwenye mechi za kirafiki na Kombe la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), au Azam Sports Federation Cup (ASFC) kutokana na maumivu hayo.

Simba SC ilishinda 3-0 dhidi ya wenyeji, Polisi Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma na 1-0 mara mbili dhidi ya Madini FC Uwanja wa Sheikh Amri Abeid na dhidi ya Mererani Stars Uwanja wa CCM Mererani, Arusha.

Daktari wa Simba, Yassin Gembe amesema kwamba baada ya timu kurejea kutoka Arusha wanatarajia Mwanjali atarejea kikosini.

Gembe alisema walitaka Mzimbabwe huyo apumzike kwa mwezi wote wa Machi ili awe fiti zaidi kuliko kumharakisha kurejea uwanjani.

“Lengo la kumpa mapumziko marefu ni kutaka apone vizuri ndiyo aanze mazoezi, tunaamini kwa sasa atakuwa tayari kabisa,”alisema Gembe.

Mwanjali aliumia goti katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Prisons Februari 11, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Simba ikishinda 3-0.

Mwanjali aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC, alitolewa kwa machela siku hiyo na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Mwinyi Kazimoto dakika ya 62.

JPM amteua Mwakyembe kuwa Waziri wa Habari
Video: Polisi wanaswa wakiiba mafuta ya ndege za JPM, Uamuzi mgumu kwa Makonda