Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli amempongeza Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila kwa hatua aliyoichukua kuwachapa viboko wanafunzi 14 wa Shule ya Sekondari Kiwanja wilayani Chunya mkoani humo na kuwasimamisha masomo wanafunzi 392, waliokutwa na simu na wanaotajwa kuwa chanzo cha kuchomwa mabweni mawili ya shule hiyo.

Rais Magufuli ametoa pongezi hizo leo akiwa katika ziara yake mkoa wa Songwe ambao ni jirani na mkoa wa Mbeya, na akatangaza kuwa amewafukuza wanafunzi wale na kuvunja Bodi ya shule hiyo.

“Nilikuwa nazungumza na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya nikamwambia ulitakiwa uwatandike viboko kwelikweli na uwafukuze shule. Na natangaza hapa kuwa wale wanafunzi wote wamefukuzwa shule na Bodi ile imevunjwa kwa sababu ni uzembe wa Bodi hadi mambo yale yametokea,” alisema Rais Magufuli.

“Nimempongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuwatandika viboko wale wanafunzi, haiwezekani tunajenga shule watoto wanachoma. Nimemwambia fukuza fomu 5 na 6 na wamefukuzwa. Eti haki za binadamu, haki za binadamu watoto wawe na viburi vya kipumbavu? Hao wa haki za binadamu wakajenge sasa mabweni,”aliongeza.

Mkuu wa mkoa huyo aliwasimamisha masomo wanafunzi hao tangu Oktoba 3, 2019 hadi Oktoba 28, 2019 na kuwapa wanafunzi 392 masharti ya kulipa Sh 200,000 kila mmoja warejeapo shuleni hapo kwa lengo la kurejesha gharama za ukarabati wa mabweni yaliyochomwa moto.

Aidha, RC Chalamila aliwataka wanafunzi 14 kuhakikisha wanalipa Sh 500,000 kwa ajili ya kurejesha gharama za ukarabati wa mabweni na pia warudi shuleni hapo na wazazi wao.

Meddie Kagere asukiwa mkakati wa kuihama Simba
Miraji Athumani ampiku Meddie Kagere VPL