Mambo huenda yakawa magumu kwa meneja wa klabu ya Chelsea, katika juma hili kufuatia mawasiliano kati yake na mmiliki wa klabu ya Chelsea kukatika, kutokana na mwennedo mbovu wa kikosi cha klabu hiyo ya magharibi mwa jijini London.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Sunday Express, umebaini Roman Abramovich amekata mawasiliano na meneja huyo kutoka nchini Ureno, tofauti na ilivyokua siku za nyuma ambapo wawili hao walishibana katika utendaji wa kazi na kutakana ushauri.

Hali hiyo imechukuliwa kama mwisho wa Jose Mourinho, ambaye alionekana kuvumiliwa kwa matokeo mabaya ambayo amekua akiyapata msimu huu, lakini tangu kufungwa kwa timu ya Chelsea mwishoni mwa juma lililopita kwenye uwanja wa Britannia, Abramovic ameonyesha kuchoshwa na hali hiyo.

Hata hivyo haijaelezwa kwa kina, kama kuna vikao vinaendelea ndani kwa ndani kwenye klabu ya Chelsea kuhusu mustakabali wa Jose Mourinho, lakini tabia ya mmiliki wa klabu hiyo imekua ikidhihirisha wazi anapofikia hatua ya kukata mawasiliano na aliye karibu naye, huwa kuna viashiria vya kuachana na muhusika.

Chelsea ilipoteza mchezo wa mwishoni mwa juma lililopita kwa kufungwa bao moja kwa sifuri dhidi ya Stoke City, ambapo Jose Mourinho hakuwepo kwenye benchi la The Blues, wala hakuingia uwanjani kutokana na adhabu aliyopewa na chama cha soka nchini England FA, pamoja na kutozwa faini ya pauni elfu hamsini.

Kwa matokeo hayo Chelsea imeendelea kuwa katika nafasi za chini kwenye msimamo wa ligi ya nchini England, baada ya kujikusanyia point 11 katika michezo 12 waliyocheza mpaka sasa.

Chadema Watishia Kuhamasisha Mgomo Wa Wanafunzi Waliokosa Mikopo
Nigeria Mabingwa Wa Dunia U17 2015