Mbunge wa jimbo la Kibamba, John Mnyika ameeleza kutoridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa alipofanya ziara yake katika maeneo yanayohudumiwa na mitambo ya Ruvu Juu hivyo amemuomba Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Kuingilia kati na kuchukua hatua stahiki.

Hii ndiyo taarifa yake kwa vyombo vya habari:

Sijaridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Waziri wa Maji alipofanya ziara juzi na kunukuliwa na vyombo vya habari jana. Hivyo, naomba Waziri Mkuu achukue hatua zifuatazo:

Mosi, atake Wizara ya Maji impatie nakala ya ripoti ya uchunguzi kuhusu kukatikakatika mara kwa mara kwa maji katika mitambo na maeneo ambayo yanahudumiwa na mitambo ya Ruvu juu. Baada ya kupata ripoti hiyo atembelee katika DAWASA/DAWASCO na ‘kutumbua majibu’ ya ufisadi na udhaifu uliopo.

Pili, atembelee ujenzi unaoendelea kwenye chanzo cha Ruvu juu ambao ulipaswa kukamilika toka 2013 lakini haijawa hivyo, na katika mkutano wa mwisho wa Bunge la Kumi Wizara ya Maji iliahidi ungekamilika Agosti 2015 na haijawa hivyo pia.

Tatu, atembelee eneo la ulazaji wa Bomba kubwa jipya kutoka Mlandizi mpaka Kimara na ujenzi wa matenki mapya ambao ulipaswa kukamilika 2013, lakini haijawa hivyo, na katika mkutano wa mwisho wa Bunge la Kumi Wizara ya Maji iliahidi ungekamilika Septemba 2015 na haijawa hivyo pia.

Nne, ulazaji wa mabomba ya kusambaza maji katika maeneo yasiyokuwa na “mabomba ya mchina” katika kata za Kibamba, Kwembe, Mbezi, Msigani, Saranga, Goba haujaanza kabisa. Naomba ufuatilie mchakato wake wa mkataba na vyanzo vyake vya rasilimali ili kazi hiyo ianze sanjari na bomba kuu linalolazwa ili yakamilike kwa pamoja wananchi wapate maji.

Achukue hatua zingine za ziada kwa kurejea hoja binafsi niliyoiwasilisha Bungeni tarehe 4 Februari 2013 (nimeambatanisha nakala) ambayo maelezo yake na mapendekezo yake bado ni muhimu yakafanyiwa kazi.

Uchaguzi Zanzibar: Jaji Bomani Amshangaa Jecha
Sasa Ni Rasmi, Chelsea Yamfungashia Virago Mourinho