Mwanatheolojia mkongwe na waziri mstaafu wa Kanisa la Presbyterian Church of East Africa (PCEA), Mchungaji Timothy Njoya, amesema Rais wa zamani Uhuru Kenyatta anahitaji kuitwa ili kupatanisha mvutano kati ya mrithi wake, William Ruto, na kiongozi wa Azimio La Umoja Raila Odinga.
Amesema hayo wakati wa mahojiano na kituo cha habari cha Citizen nchini Kenya ambapoa amesema wakenya walipigana vikali kuunda kile alichokiita uwanja sawa wa kuchezea, akipendekeza Kenyatta aletwe kwenye bodi ili kusimamia mchezo huo.
“Tulipigania uwanja sawa wa kuchezea na kuwa na mwamuzi mzuri. Eti tungekuwa na mwamuzi mzuri Kenya, ningesema Uhuru angekuwa mwamuzi bora. Anasifika kwa kile alichokifanya, kwenda Kongo katika mzozo unaoendelea, kwa kuteuliwa na Ruto,” akasema kasisi huyo mkongwe.
Mchungaji Njoya, ambaye alikuwa akipinga siasa za chama kimoja cha rais wa pili wa Kenya, Daniel Moi, amesema mchezo huo hauna mwamuzi wala sheria.
“Nchini Kenya hivi sasa, tuna vyama viwili vikuu; shirikisho la kandanda la Raila Luo-Kamba, ambalo linacheza mchezo na shirikisho la Ruto la Kikuyu-Kalenjin. Mechi hiyo haina refa na niko hapa kuwaambia wanamhitaji,” amesema Njoya
Kenyatta ni Mwezeshaji wa Mchakato wa Nairobi unaoongozwa na EAC kuhusu Urejeshwaji wa Amani na Utulivu mashariki mwa DRC, na amekuwa akisimamia ujumbe unaojadili urejeshaji wa usalama katika nchi hiyo yenye matatizo ya Afrika ya Kati.
“Amekwenda kama Mkenya, si kama kiongozi wa chama chochote. Anapatanisha maeneo kama Somalia. Anachofanya, anafaa kuwa anafanya nchini Kenya,” Njoya alisema.
“Nani anaweza kumwambia hivyo? Anaweza tu kuambiwa na kanisa, ambalo linaweza kwenda kumwambia Mama Ngina, ambaye ni mama wa taifa, aende kumwambia mwanawe kwamba yeye ni mzee wa serikali kama rais wa zamani. Sasa anafaa kuwa mwamuzi wa mchezo kwa sababu amekuwepo,” alisema Njoya.
Raila Odinga, alishindwa na Ruto katika kinyang’anyiro kikali cha urais mwezi Agosti mwaka 2022, amekuwa akizunguka nchi nzima kuwahamasisha wafuasi kukataa utawala wa Rais Ruto, huku akisema kura zilivurugwa na kutaka Ruto na viongozi wote serikalini wajiuzulu.