Hali mbaya iliyonayo Mtibwa Sugar inayoburuza mkiani kwa pointi tano, ikishinda mechi moja, sare, sare mbili na kupigwa saba katika michezo yao 10, hilo linamfanya kocha wa timu hiyo, Zuber Katwila kuumiza kichwa.

Katwila amesema kuwa; “Hali ni mbaya, pamoja na hayo yote tupo kwenye mapambano makali ambayo lazima akili zifanye kazi sana na siyo kukata tamaa, Ligi Kuu ina ushindani hakuna cha kupata matokeo nyumbani wala ugenini, kikubwa ni kuendelea kukomaa hadi mwisho.”

“Najitahidi kujenga akili za wachezaji wasione huu ndio mwisho wao, bado kuna nafasi kubwa ya kupanda nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu,najua nafasi tuliopo kila mmoja inamuumiza, ila hatuwezi kuishia kuumia lazima tuchukue hatua ya kutupa furaha.”

Kwa upande wa Mlinda Lango wa timu hiyo, Mohamed Makaka amesema wanapambana kwa kadri wawezavyo kabla mambo hayajawa magumu zaidi kuondoka mkiani; “Tuna kazi ngumu ila hutatakata tamaa hadi kieleweke, nina imani tutaondoka mkiani na kuwapisha wengine.”

Kinara wa mabao matatu ndani ya timu, Matheo Anthony amesema “Kuna wakati hata usingizi unakata ukiwaza nini kifanyike ili kuondokana na ugumu wa kupata matokeo ya ushindi.”

Jumla ya mabao ya kufunga ya timu hiyo ni 10 wafungaji Matheo (matatu), Rashid Karihe (mawili), Kassim Haruna (bao moja), Abdul Hilal (bao moja), Abalkassim Suleiman (bao moja), Ladeki Chasambi (bao moja) na Juma Nyangi (bao moja).

Mechi nne zijazo za Mtibwa ni dhidi ya Tabora, Namungo, Young Africans na Mashujaa. Timu hiyo imeambulia pointi moja kwenye mechi nne za ugenini.

Waziri Silaa aikataa dhambi mbele ya Mchungaji
Ahmed Ally afichua ujio wa Benchikha