Baraza la Ukunga na Uuguzi Tanzania, (TNMC) limeviomba vyombo vya ulinzi na usalama nchini kumkamata popote alipo muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Igunga Mkoani Tabora, Damian Mgaya (41) aliyetoroka Hospitalini hapo kufuatia tuhuma za kumbaka mgonjwa ambaye ni binti wa miaka 16 kuanzia saa nne usiku hadi saa nane.

Ambapo mara baada ya kumaliza kumbaka binti huyo aliamua kumtupa eneo la kufulia nguo kwenye nyasi akiwa hajitambui na kumwagia maji mwili mzima.

Mama mzazi wa binti huyo ametoa taarifa hiyo akisema siku ya tukio muuguzi huyo alifika katika wodi namba 3 na alipoona mgonjwa hali yake si nzuri aliomba aondoke nae ili akambadilishie dawa, walipofika ofisini kwake alimchoma sindano ya usingizi na kisha kumbaka.

Mganga Mkuu wa Wilaya hiyo amethibitisha tuhuma hizo na kusema kesi imefikishwa katika kituo cha polisi.

“Ni kweli tukio lipo na sio mara ya kwanza siku za nyuma Mgaya akiwa kituo cha afya cha Tarafa ya Igurubi alifanya tukio kama hilo, hii ni mara ya pili na huu ni ukiukwaji mkubwa wa taratibu na kanuni za kiutumishi”- Dkt.Ruta Deus, Mganga Mkuu wa Wilaya.

Kufuatia mtiririko wa matukio hayo kufanywa na muuguzi huyo, Baraza la Uuguzi na Ukunga Tanzania, (TNMC) limeamua kumchukulia hatua ya kusimamisha leseni yake ya kutoa huduma za ukunga na uuguzi popote nchini Tanzania kwa muda wa miezi mitatu.

 

RC Chalamila atangaza bakora kwa wasioa na kuolewa Mbeya
BAKITA yatoa maana ya neno Kisulisuli