Hakika mapenzi hayana mbabe wala ‘gym’ ya kujifua kwa ajili ya kuyakomesha yanapoanza vitimbwi. Pamoja na uzuri, utajiri na mvuto wa rapa Nicki Minaj ni miongoni mwa wasichana warembo walionyaswa vibaya kwenye mapenzi.

Nicki amesababisha huzuni kwa mashabiki wake kupitia vipande vya video ya kutangaza kipindi chake cha Queen, inayomuonesha akisimulia jinsi ambavyo aliishia kuwa mhanga wa manyanyaso ya mapenzi baada ya kuukabidhi moyo wake kwa wanaume aliowapenda.

Kupitia video hizo, rapa huyo alianza kusimulia jinsi alivyokuwa anashuhudia baba yake akimnyanyasa mama yake kwa vipigo na matusi. Malikia huyo wa michano amesimulia kuwa kuna wakati alilazimika kuingilia kati ugomvi huo kumlinda mama yake.

 Alisema kuwa kutokana na kushuhudia manyanyaso hayo akiwa msichana mdogo, aliapa kutomruhusu mwanaume kumfanyia hivyo lakini aliporuhusu moyo wake kupenda, mambo yalibadilika.

“Niliapa tangu nikiwa na umri ule kuwa hakuna mwanaume ambaye ataninyanyasa, kuniita majina ya ajabu, na kunitenda kama vile. Lakini ghafla, hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu,” alisema Nicki akitokwa machozi.

Alieleza kuwa manyanyaso hayo yalimfanya hata kushindwa kukosa kujiamini katika muziki wake kwani alijua ndani yake hana kitu.

“Nilimruhusu binadamu mmoja kunifanya niwe chini sana, kiasi kwamba hata nilisahau nilikuwa nani. Nilikuwa naogopa hata kuingia studio. Nilikuwa sijiamini,” aliongeza.

Ingawa hakutaja majina ya wanaume waliomtendea hivyo, mashabiki wengi walianza kumnyooshea kidole rapa Meek Mill ambaye alikuwa mpenzi wake na walipigana chini mapema mwaka 2017.

Meek naye ametumia mtandao wa Instagram kuweka jumbe ambazo zinaaminika kuwa ni majibu kwa Nicki, “wakibanwa watakimbilia kudai kuwa wao walikuwa wahanga.” Aliendelea kwa maelezo mengi akidai kuwa watu hao wanachotafuta ni huruma ya mashabiki wao.

 

View this post on Instagram

 

Lol

A post shared by Meek Mill (@meekmill) on

Hivi sasa mkali huyo wa ‘Chu Li’ anasadikika kuwa na uhusiano wa kimapenzi na dereva wa mbio za magari Formula 1, Lewis Hamilton baada ya kuwepo taarifa kuwa alikuwa na uhusiano kwa muda mfupi na Nas.

Ndege za jeshi zagongana, uwanja wafungwa
Madiwani wa CCM, Ukawa wapigana ngumi