Beki wa klabu bingwa nchini Hispania FC Barcelona, Gerard Pique amewataka radhi mashabiki wa klabu hiyo pamoja na wadau wa soka duniani kote kufuatia adhabu ya kadi nyekundu iliyomkuta wakati wa mchezo wa mkondo wa pili wa kuwania Spanish Super Cup uliochezwa usiku wa kuamkia jana huko Camp Nou.

Pique, alionyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 56, ambapo imeripotiwa alimtusi muamuzi, baada ya kuchukizwa na maamuzi yaliyochukuliwa dhidi ya klabu yake ya Barcelona.

Vyombo kadhaa vya habari nchini Hispania vimeeleza kwamba, muamuzi katika mchezo huo, Carlos Velasco Carballo aliwasilisha ripori yake kwenye mamlaka ya soka nchini humo na kuelezea sababu za kuchukua maamuzi ya kumuadhibu beki huyo kwa kadi nyekundu.

Ripoti hiyo ya muamuzi, imeeleza kwamba Pique alimtolea lugha chachu ambayo alishindwa kuivumilia, hatua ambayo ilimpa msukumo kuchukua maamuzi ya kumuonyesha kadi nyekundu.

Hata hivyo Pique, amekanusha kumtusi muamuzi huyo, kwa kusema huenda ilikua ni mbinu za kutaka kutimiza wajibu wa kumuadhibu kwa kadi nyekundu.

Kutokana na adhabu hiyo beki huyo mwenye umri wa miaka 28, shirikisho la soka nchini Hispania limefanya maamuzi ya kumfungia michezo minne ya ligi kuu ya nchini humo  ambayo inatarajia kuanza kutimua vumbi lake mwishoni mwa juma hili.

Berahino Apigwa Stop Kujiunga Na Spurs
Twiga Stars Kujipima Ubavu Na Kenya Jumapili