Mamlaka ya Kudhibiti Ununuzi wa Umma nchni (PPRA), imeeleza kuwa utumiaji wa utaratibu wa kikosi kazi “ Force Account “katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ni njia inayofaa ikiwa itasimamiwa vyema.

Hayo yalibainishwa katika utafiti mdogo uliofanywa na Mamlaka, ili kuangalia ufanisi wa utumiaji wa kikosi kazi katika miradi ya maendeleo ya ujenzi inayoendelea hapa nchini uliohusisha miradi 175 iliyofanywa kwa njia ya kikosi kazi .

Meneja Utafiti na Nyaraka wa Mamlaka Mhandisi, Nashon Masunya alieleza kuwa hivi karibuni kumekuwa na ongezeko la matumizi ya njia ya kikosi kazi katika miradi ya umma hasa katika ujenzi wa shule, vituo vya afya, majengo ya Serikali na ujenzi wa nyumba zinazomilikiwa na Serikali.

Moja ya shule ya sekondari Halmashauri ya Kahama inayojengwa kwa kutumia nguvu kazi “Force account” . Ujenzi huo unatekelezwa kwa kupitia mradi wa SEQUIP

Alisema, ongezeko hilo limepelekea baadhi ya maeneo hoja nyingi kuibuliwa juu ya ukiukwaji wa maadili ya ununuzi na usimamizi wa mikataba na hivyo kupelekea matumizi makubwa ya fedha wakati wa utekelezaji wake.

Mhandisi Masunya, alieleza utafiti huo ulilenga kuangalia thamani ya fedha (Value for Money) na kuona endapo njia hiyo ni njia sahihi kwa matumizi ya kutekeleza miradi ya maendeleo, ili kuiwezesha Mamlaka kutoa ushauri sahihi kwa Serikali na wadau wengine wa maendeleo juu ya matumizi ya kikosi kazi.

“Tuliamua kufanya utafiti ili tuone kama njia hiyo ya Force Account ni salama kutumiwa na Serikali kutokana na hoja nyingi zinazoibuliwa sio tu na viongozi bali hata wananchi” Alisema.

Mhandisi Masunya aliongeza kuwa yapo maeneo yaliyofanikiwa katika utekelezaji wa miradi kwa kutumia njia hiyo licha ya mengine kushindwa kufanya vizuri na kwamba PPRA ndiyo Mamlaka yenye wajibu wa kusimamia ununuzi wa Umma nchini, hivyo ina wajibu wa kuhakikisha thamani ya fedha na uwazi katika ununuzi unaonekana.

Akieleza zaidi kuhusu njia hiyo alisema Sheria imeweka wazi kuwa yapo mazingira yanayo weza kulazimu taasisi kutumia njia hiyo. Mazingira hayo ni kama taasisi inayotaka kutekeleza mradi inaona kazi hiyo sio kubwa na maeneo ya mradi huo ni mbali kufikika.

Mhandisi Masunya alizikumbusha taasisi kuwa kigezo cha muhimu ni lazima zihakikisha kuwa wapo wataalamu ndani ya taasisi wanaoweza kusimamia na kuifanya kazi hiyo kwa ufanisi.
Utafiti huo ulijumuisha miradi iliyofanywa katika sekta ya afya, maji na elimu kwa kutumia fedha za UVIKO – 19.

Utafiti huo, uliangalia pia pia kaguzi maalum zilizofanywa na Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa fedha za Serikali (CAG) katika miradi ya sekta ya Elimu kwa mwaka 2020 na Kaguzi maalum zilizofanywa na PPRA katika sekta ya afya mwaka 2020.

Ifahamu mbinu ya kuwa na bahati nzuri maishani mwako
Waziri Kairuki akemea Viongozi waomba rushwa