Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia ombi la kumegwa eneo la ekari 100 lililokuwa linamilikiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kwa ajili ya ujenzi wa Zahanati ya Kata ya Mninga iliyopo wilayani Mufindi mkoani Iringa.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt.Pindi Chana wakati akizungumza na wananchi wa Kata ya Mninga Wilayani Mufindi Mkoani Iringa, na kusema uamuzi huo wa Rais Samia umetokana na yeye kuguswa na kujali afya na maendeleo ya maisha ya wananchi wake.
Amesema, eneo hilo lililomegwa ni moja ya sehemu ya Shamba la Miti la Sao Hill ambalo lina miti ya kupandwa aina ya misindano yenye zaidi ya miaka mitano lakini hata hivyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekubali eneo hilo ijengwe zahanati ili wananchi wasisafiri umbali mrefu.
Katika hatua nyingine, Waziri Balozi Dkt.Pindi Chana amewataka wananchi hao kuacha kusafisha mashamba kwa kutumia moto hali ambayo imekua chanzo cha moto pale unaposhindwa kudhibitiwa na kusababisha hasara .
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mufindi, Diwani wa Kata ya Mninga, Festo Mgina amesema anamshukuru sana Rais Samia kwa kukubali ombi la wananchi wa Mninga lililowasilishwa kupitia Halmashauri ya Mufindi na kusisitiza kuwa Zahanati hiyo itawapa ahueni wananchi wake waliosumbuka kwa muda mrefu.