Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemteua Juma Muhimbi kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya.

Kabla ya uteuzi huo Muhimbi alikuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Transparent Finacial and Tax Consulting Services Ltd ya Dar es Salaam na anachukua nafasi ya Anne Makinda ambaye muda wake umemalizika.

Dkt. Edmund Mndolwa ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya Posta Tanzania (TPB) , ambapo anaendelea na wadhifa huo baada ya kumaliza kipindi chake cha kwanza.

Rais Samia pia amemteua Profesa John Kondoro kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Reli Tanzania (TRC), ambapo naye anaendelea na wadhifa huo baada ya kumaliza kipindi chake cha kwanza.

Profesa Valerian Silayo kutoka Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), ameteuliwa na Rais kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC).

Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais , Ikulu imeeleza kuwa Uteuzi wa Wenyeviti hao umeanza leo Juni 16, 2021.

Amuua mkewe kwa kisu na kujilipua kwa petroli baada ya wazazi kumkataa mkewe
Jeshi la Polisi ladaka heroin kilo 7.73