Wenslausi James (30) na Betha Kasimili (25), ambao ni wakazi wa kijiji cha Busongo kata ya Mwamashele wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, wamefariki dunia baada ya mwanaume huyo kujilipua kwa moto kwa kutumia mafuta ya Petroli, kwa madai ya wazazi wa mwanaume kumkataa mwanamke.

Kwa Mujibu wa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoani Shinyanga, Kamishina msaidizi wa Polisi, Jackson Mwakagonda, tukio hilo limetokea June 14 mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi.

Mwakagonda amesema wanandoa hao walikuwa wamezaa watoto watatu, lakini wazazi wa mwanaume walimkataa mke wake, na kuamua kuuvunja mji pamoja na kurudisha mahari nyumbani kwao na mwanamke.

Aidha, amesema baada ya mji huo kuvunjika, ndipo mwanaume akasikia kuwa mke wake anataka kuolewa, na kuamua kwenda nyumbani kwa kina mwanamke akiwa na dumu la mafuta ya Petroli lita tano, na kisha kuingia chumbani kwa mwanamke na kufunga mlango na kisha kuanza kugombana.

“Mwanaume huyu alimchoma kisu cha ubavuni mke wake, na kisha kumfunga minyororo na kumwagia mafuta ya Petroli, kisha na yeye kujimwagia Petroli akawasha kiberiti na kujilipua moto, ambapo waliteketea pamoja na nyumba,” amesema Mwakagonda.

Aidha Kamanda ametoa wito kwa wazazi, kuacha kuingilia ndoa za watoto wao, pamoja na wanandoa kuacha kujichukulia sheria Mkononi, na pale penye migogoro bali watafute ufumbuzi kwa kufuata sheria.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Juni 17, 2021
Rais Samia ateua Wenyeviti wa Bodi, Anne Makinda astaafu