Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla amewataka Madiwani wa Jiji la Dar es salaam kuepuka migongano na mivutano isiyokuwa na faida yoyote kwa Wananchi na badala yake wajikite katika kujenga hoja na mipango ya kutatua kero kwa maslahi mapana ya Wananchi.

RC Makalla amesema kumekuwa na tabia ya ajabu pale Serikali inapotoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi fulani kisha madiwani wanajikuta wanaanza kulumbana kwa mambo yasiyokuwa na msingi, jambo linalochelewesha kuanza kwa miradi ya maendeleo na kuleta usumbufu kwa Wananchi.

Akizungumza wakati wa kikao cha pamoja kati yake na Madiwani pamoja na Maafisa Watendaji kata, Makalla amewataka viongozi hao kusimamia kikamilifu suala la usafi katika maeneo yao na kuwa mstari wa mbele kwenye usimamizi wa miradi ya maendeleo.

Aidha, Makalla ameonyesha kufurahishwa na mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana katika Operesheni tokomeza Majambazi na Vibaka Dar es salaam ambapo amewahakikishia wananchi kuwa Serikali imejizatiti kuwalinda na mali zao.

Hata hivyo, Makalla amelitaka Jiji la Ilala kuhakikisha linawapanga vizuri machinga katika maeneo yao ili waweze kufanya biashara zao kwa hali ya usalama na kwa mujibu wa sheria.

Makalla amelitaka Jiji la Ilala kuhakikisha Mradi wa Machinjio ya kisasa Vingunguti unaanza kufanya kazi ifikapo Julai Mosi ili lengo la kuanzishwa kwa machinjio hayo litimie.

Kwa upande wao Madiwani na Maafisa Watendaji Kata wamemuhakikishia RC Makalla kuwa maelekezo na maagizo aliyoyatoa wameyapokea kwa mikono miwili na watayafanyia kazi kuanzia leo.

Aidha, wamempongeza kwa uamuzi wake wa kuanza ziara ya Kata kwa Kata na wamemuahidi kumpatia ushirikiano kwa kuwa wanaamini kupitia ziara hiyo watu wengi watatatuliwa kero zao.

Breaking News: IGP Sirro apangua Makamanda, Muliro RPC mpya Dar
Fimbo ya ECOWAS yaichapa Mali