Kocha Mkuu wa klabu ya Red Arrors FC ya Zambia Chisi Mbewe, ameanza kujihami kuelekea mchezo wa Mkondo wa kwanza wa Hatua ya Mtoano Kombe la Shirikisho barani Afrika, utakaowakutanisha dhidi ya Mabingwa wa Tanzania Bara Simba SC mwishoni mwa juma lijalo.

Simba SC itaanzia nyumbani Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam katika mchezo huo, kisha itakwenda kumalizia mchezo wa mkondo wa pili nchini Zambia mwanzoni mwa mwezi Desemba.

Kocha Mbewe amesema wanafahamu Klabu ya Simba ina falsafa ya kipekee inapocheza nyumbani, hasa kuwa na Mashabiki wengi wanaojitokeza Uwanjani na kuwashangilia kwa nguvu, hivyo wanajiandaa na hali hiyo ili waweze kupambana ugenini kwa kujiamini.

“Tunajua Falsafa ya watanzania ni kujitokeza wengi sana uwanjani ili kuzisapoti timu zao ila sisi tumejipanga zaidi uwanjani ,malengo yetu msimu huu ni kufika robo fainali ya kombe la shirikisho na tunaweza kufanya hivyo” amesema Kocha Mbewe

Simba SC iliangukia hatua ya mtoano Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kwa kufungwa mabao 3-1 dhidi ya Jwaneng Galaxy, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Kabla ya mchezo huo Simba SC ilishinda ugenini mjini Gaborone-Botswana mabao 2-0.

Gadiel Michael: Tunaiheshimu Ruvu Shooting
Didier Gomes atusua Mauritania