Rais wa Kenya William Ruto amesema katika utawala wake hatamteua mwanachama yeyote wa upinzani kwa kuwa hali hiyo itadhoofisha Upinzani.

Akizungumza mjini Naivasha katika mkutano wa kundi la wabunge wa Kenya Kwanza, rais alisisitiza kwamba anataka chama cha upinzani chenye nguvu ambacho kitasaidia kuhakikisha serikali yake inafanya kazi kwa uthabiti.

Ruto alisema upinzani mkali, unaweza kuendesha serikali inayowajibika.

“Hatutamteua mwanachama yeyote wa upinzani kwa sababu tunataka upinzani mkali, tunataka upinzani ambao utaiweka serikali kwenye udhibiti Mkali. Tunataka kuendesha serikali inayowajibika; hatuna cha kuficha,” alisema.

Kwa upande wa kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga amewakosoa Majaji wa Mahakama ya Juu kuhusu jinsi walivyoshughulikia kesi ya uchaguzi wa urais wa 2022.

Akiongea mjini Machakos Ijumaa, Septemba 16, wakati wa mkutano wa viongozi waliochaguliwa Azimio, alisema kuwa, majaji wa Mahakama ya Juu, walijazwa chuki.

Aliendelea na mashambulizi yake makali dhidi ya Jaji Mkuu Martha Koome, akimshutumu kwa kutumia lugha ya kudhalilisha katika uamuzi ulioidhinisha ushindi wa William Ruto.

“Wakati wowote majaji wanapotumia maneno makali kwa mawakili, ni matokeo ya kuvurugika fahamu. Mahakama Kuu sasa iko kwenye siasa. Mimi naamini uamuzi huo uliongozwa na shetani,” alisema.

CWT yawasimamisha kazi viongozi wakuu
Pikipiki yauwa Watanzania watatu Kenya