Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali itaendelea kufuatilia miradi yote inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini, ili kudhibiti matumizi mabaya ya mali ya umma.
Majaliwa, ameyasema hayo hii leo Februari 9, 2023 Bungeni jijini Dodoma, wakati akijibu swali la Mbunge wa Arumeru Magharibi, Noah Saputu aliyetaka kujua kauli ya Serikali kuhusu wizi na ubadhirifu katika miradi ya umma.
Amesema, Serikali kupitia ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa mfumo wa ufuatiliaji na tathmini ya mipango na shughuli za Serikali na sasa watendaji wake wanapita katika mamlaka za Serikali ili kufanya tathimini, kujiridhisha kuhusu thamani ya fedha katika miradi inayotekelezwa.
Aidha, Waziri Mkuu amesema Serikali ina mfumo wa kufanyia tathmini na mapitio ya mwenendo wa matumizi ya mali na fedha za umma, pamoja na kufanyia kazi mapendekezo ya taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), inayotolewa baada ya kufanya ukaguzi ili kubaini mapungufu kwenye baadhi ya miradi.