Vilabu 14 vya Pemba ambavyo viligoma kucheza ligi kuu ya Zanzibar kwa madai ya kukiukwa kwa katiba ya ZFA, vilabu hiyo sasa vimekubali kwa kauli moja ya kucheza ligi hiyo, itakayoanza kutimua vumbi lake Machi 15 mwaka huu.

Vilabu hivyo vimesema kwa sasa viko tayari kwa siku kuicheza michezo minne, miwili Mchana na jioni kutokana na ligi hiyo kuchezwa katika viwanja viwili tofauti.

Alivitaja vilabu vilivyoshiriki katika kikao hicho kuwa ni pamoja na Jamhuri, Mwenge, Kizimbani, Chipkizi, Hard Rock, Aljazira, Okapi, Sharp Victor, Fufuni, Afican Kivumbi, Shaba, Madungu na Dogomoro.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi mara baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha Vilabu na wajumbe wa Kamati Tendaji ya ZFA Pemba, Shabani Ali Mbwanda alisema vilabu kwa kauli moja vimekubali kucheza ligi kwa sasa.

Shabani alisema kwa sasa vilabu vimejipanga vizuri, kuhakikisha ligi hiyo inachezwa na kurudisha heshima ya Kisiwa cha Pemba, kushiriki katika mashindano makubwa ya kimataifa.

Hata hivyo alisema watahakikisha wanawahi kalenda ya FIFA, CAF, TFF na ZFA kuhakikisha wanamaliza kwa wakati ligi hiyo, licha ya kuwa wako katika kipindi kifupi.

Kwa upande wake Makamo wa Rais wa ZFA Taifa Pemba, Ali Mohamed Ali alisema matayarisho yote ya kuanza kwa ligi hiyo yameshakamilika kilichobakia ni kusubiriwa kwa siku ya ufunguzi wake.

Alisema vilabu vitakavyofungua dimba ya ligi hiyo ni Aljazira na Kizimbani katika Uwanja wa FFU Finya, huku Katika uwanja wa Gombani Jamhuri na Chipukizi zitatoana jasho kiwanjani hapo.

Machi 20 hadi 22 hakutakuwa na michezo yoyote ya ligi hiyo, kutokana na kuwepo kwa uchaguzi mkuu wa marudio na baada ya hapo ligi hiyo itaendelea tena.

Aliwataka waamuzi kuhakikisha wanafuata sheria 17 za soka kwa kuchezasha vyema ligi hiyo bila ya upendeleo wowote, ili kuhakikisha kila mwenye uwezo anapata haki yake.

(Chanzo  Abdi Suleiman, PEMBA.)

Jux aweka wazi mtego uliotumika kunasa penzi la Vanessa Mdee, ni ‘kadude’
Ubunifu: Baada ya 'walimu na dadala bure', Makonda aja na mradi wa ‘mtaa wa baa’