Tanzania inatarajia kunufaika na mradi wenye thamani ya Shilingi 120 Bilioni kwa ajili ya miradi ya uhifadhi wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi, kutoka Mfuko wa Mazingira wa Dunia (GEF).
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Bi. Mary Maganga ameyasema hayo hii leo Februari 13, 2023 Jijini Dodoma na wakati akifungua Warsha ya siku mbili ya Wadau na Wataalamu wa Mazingira inayolenga kuainisha vipaumbele vya miradi ya mazingira na mabadiliko ya tabianchi inayosimamiwa na GEF.
Amesema, “Tanzania ni nchi mnufaika wa miradi ya GEF ambayo inafadhiliwa kupitia mikataba mbalimbali ya kimataifa, hivyo Ofisi ya Makamu wa Rais imeona umuhimu wa kuita wadau na wataalamu kutoka wizara na taasisi za kisekta kutoka mashirika mbalimbali ili kuweka mikakati ya pamoja na kufanikisha ajenda ya mazingira.”
Aidha, amewataka wadau na wataalamu hao kutumia vyema ujuzi na uzoefu walionao katika kuimarisha mapambano na changamoto za mazingira zilizopo kwa lengo la kuhakikisha maandalizi na utekelezaji wa miradi chini ya GEF- awamu ya nane inatekelezwa kwa wakati.
Kwa upande wake Mratibu wa GEF – Kanda ya Afrika, Ibrahima Sow alisema kuwa Tanzania imetengewa mgao huo wa fedha za mzungumzo wa nane katika maeneo matatu ya mradi kwa kipindi cha miaka minne ijayo.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni mradi wa usimamizi katika Maziwa Makuu na Mabonde ya Maji, fedha za kujenga uwezo kwa wataalamu wa miradi pamoja na usimamizi wa miradi katika nchi zinazoendelea.
Naye Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Andrew Komba alisema kuwa katika eneo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, Serikali imeendelea kushirikiana na wadau mbalimbali na kuhimiza na kuhamasisha utunzaji wa mazingira.