Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekabidhi rasmi msaada wa kibinadamu kwa Serikali ya Malawi, kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa kimbunga Freddy kilichosababisha mafuriko yaliyoikumba nchi hiyo tarehe 13 Machi, 2023 na kusababisha madhara mbalimbali ikiwemo vifo vya zaidi ya watu 400.
Msaada huo, umekabidhiwa kwa Rais wa Jamhuri ya Malawi, Dkt. Lazarus Chakwera leo Machi 20, 2023 katika hafla fupi iliyofanyika Ikulu jijini Lilongwe na kuhudhuriwa na Viongozi mbalimbali wa Malawi na Tanzania akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Nancy Tembo na Balozi wa Tanzania nchini humo, Humphrey Polepole.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Dkt. Tax amesema Rais wa Dkt. Samia ametoa msaada wa kibinadamu na salamu za pole kwa Rais Dkt. Lazarus Chakwera pamoja na wananchi wake, kwa madhara makubwa waliyoyapata kutokana na mafuriko hayo ikiwemo vifo, majeruhi, ukosefu wa makazi pamoja na uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu ikiwemo barabara.
Amesema, Tanzania kama ndugu, rafiki na jirani wa Malawi imeguswa na janga hilo na kuchukua hatua za haraka za kuratibu msaada huo kwa ajili ya kuisaidia nchi hiyo ili kuwathibitishia kwamba Tanzania ipo pamoja nao katika kipindi hiki kigumu wanachopitia.
“Mhe. Rais Samia amenituma Malawi kuwasilisha ujumbe maalum wa salamu zake za pole na msaada wa kibinadamu kwa Mhe. Rais Dkt. Chakwera na Wananchi wa Malawi kufuatia madhara ya Kimbunga Freddy. Kama ndugu zetu na jirani zetu Tanzania inasimama na Malawi katika kipindi hiki kigumu cha mpito na leo nimewasilisha msaada huo na pia kutoa pole kwa niaba ya Rais na Watanzania,” amesema Dkt. Tax.