Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Abubakar Kunenge, ameeleza kuwa Ujenzi wa Kituo cha Mabasi cha Kimataifa cha Mbezi Luis Jijini Dar es Salaam umekamilika kwa asilimia 80.
Kunenge ameeleza hayo wakati akikagua maendeleo ya mradi huo ambao amesema bado kazi ndogo ya kumalizia kabla ya kuanza kutumika rasmi na kutoa fursa za ajira mbalimbali na biashara.
Amesema kuwa stendi hiyo imejengwa kutokana na ile ya Ubungo kuzidiwa uwezo hivyo imekuwa ndogo kulinganisha na mahitaji ya watu.
Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Mkuu wa Mkoa Kunenge, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Sipora Liana, amesema ujenzi wa kituo kipya cha mabasi yaendayo mikoani na nchi jirani unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 50 za Tanzania, fedha zilizotolewa na serikali kuu kwa ajili ya miradi huo wa kimkakati.