Hatimaye aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa ametangaza kustaafu rasmi siasa baada ya chama hicho kumpokea Edward Lowassa na timu yake anayodai ni timu ya mafisadi.

Akiongea leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Dk. Slaa amesema kuwa hakushiriki katika uamuzi wa kumkaribisha Edward Lowassa katika chama hicho kama ilivyodaiwa hapo awali bali aliletewa mapendekezo hayo kutoka kwa baadhi ya viongozi wa chama hicho akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Alifafanua kuwa alihoji maswali mengi na kutaka majibu kama wangetaka akubaliane na mapendekezo yao. Suala kubwa alilohoji ni iwapo ujio wa Lowassa na watu wake ni mtaji kwa chama hicho au ni mzigo kwa chama hicho lakini hakupewa majibu.

“Niliwauliza Lowassa anakuja kama mtaji au mzigo, yaani kwa lugha ya kiingeza ni asset au liability? Lakini suala la kwamba ni asset au liability hadi tarehe 27 hawakutuletea jibu,” alisema.

Alieleza kuwa aliendelea kushikilia msimamo wake akiwataka waliokuwa wakipendekeza ampokee Lowassa akiwemo Askofu Gwajima ambaye alimtaja kama ‘mshenga’ kwenye mpango huo wa kumshawishi.

Alisema baada ya viongozi hao wa Chadema kumshawishi kuwa Lowassa angekuja na timu kubwa ya wabunge 50 walioko madarakani hivi sasa kwa tiketi ya chadema pamoja na wakuu wa wilaya kadhaa, aliwataka wamletee majina yao pamoja na sharti la kuwataka kutangaza kuhama CCM kabla ya mchakato wa kura za maoni za kuwapata wabunge.

“Niliwataka watuambie kama ni asset anakuja na nani, na wafuasi hao ni wa namna gani. Ni vijana wa mtaani, au anakuja na viongozi ambao ni serious ambao watatusaidia katika mapambano ya kweli?”

Alisema hata hivyo walishindwa kufanya hivyo na kisha kuamua kushiriki mchakato wa kura za maoni huku wakihama baada ya majina yao kukatwa jambo ambalo amedai limefanya Chadema kuendelea kupokea ‘makapi’ ya CCM.

Aliongeza kuwa hata wali0poanza kumtajia majina ya wachache walioamua kuhamia Chadema kutoka CCM aligundua kuwa ni makapi likiwemo jina moja la mtu anaeatajwa kuwa alikuwa kinara wa wizi wa kura CCM.

Anasema kuwa hata kabla ya kuingia katia mkutano wa kamati kuu ambao Lowassa alishiriki, alifanya kikao cha awali na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Tundu Lissu na Askofu Gwajima, kikao kilichodumu kwa muda wa saa tano (Kuanzia saa nne hadi saa tisa) bila mafanikio.

“Tangu mwaka 2004 sikuwahi kutofautiana na mwenyekiti wangu katika kikao chochote cha chama, na hiyo ndio siri ya uimara wetu katika chama,” alisema. Kama kuna jambo tunatofautiana tulikuwa tunaitana tunaongea kabla ya kikao na tunakubaliana, lakini siku hiyo kwa mara ya kwanza kwenye kikao tulitofautiana.

Dk. Slaa alieleza kuwa aliwahi kuandika barua ya kujiuzulu mara mbili lakini viongozi wa chama hicho walikataa kumkubalia na kumtaka kupumzika. Pia, aliwatuhumu viongozi wa chama hicho kuwa ni waongo kwa kuwa wamekuwa waliwadanganya wananchi hata pale picha zilipoonesha wako kwenye mkutano na Lowassa.

Katika hatua nyingine, Slaa aliendelea kuweka msimamo wake kuwa Edward Lowassa alishiriki kwenye ufisadi wa Richmond na Dowans na kuwa yeye ndiye aliyekuwa ‘mastermind’ wa mchezo huo na vielelezo vinaonesha.

Alitoa mfano wenye maneno makali kuhusu Chadema kumkaribisha Lowassa, akidai kuwa ni sawa na mtu kuchota ‘kinyesi’ kutoka chooni na kukihamishia chumbani kwako, huku akihoji kati ya chumba chako na kule ulikochota kinyesi ni wapi patakuwa choo.

Alisema Lowassa ndiye kinara aliyelazimisha kampuni hewa la Richmond kupewa tenda ya kufua umeme wa dharura ingawa Tathmini ya Tenda ilionesha kuwa kati ya makampuni 8 yaliyofikia hatua ya tathmini, kampuni hiyo ilikosa vigezo na kupata marks 0. Kwamba alitumia uwaziri mkuu kuhakikisha wanapata tenda hiyo iliyoitia hasara kubwa serikali.

Aidha, Dk. Slaa alisisitiza kuwa kamati Mwakyembe ilitoa ripoti ya kweli na kwamba yapo baadhi ya mambo ambayo hawakuyaweka wazi na vielelezo anavyo kwa kuwa vigogo 27 walihusika na wizi huo.

Alimtaka Lowassa kujitokeza hadharani na kutaja kwa majina ya viongozi wa ngazi za juu anaodai kuwa walishinikiza kusainiwa kwa mkataba wa Richmond badala ya kuendelea kuwaficha.

“Ajitokeze asema kwa majina hao viongozi wa ngazi za juu zaidi ya waziri mkuu ni nani na nani, aseme kwa majina kwa sababu waio juu ni Rais na makamu wa rais, nani aliyeelekeza? Amtaje,” alisema Dk. Slaa.

Mwanasiasa huyo aliyesisitiza kuwa alikuwa anaongea ukweli mtupu muda wote, aliwataka wananchi kutoamini kile anachokisema waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye hivi sasa kwa kuwa yeye pia alishiriki katika ufisadi wa aina nyingine wakati wa serikali ya awamu ya tatu.  Alimuita Sumaye kuwa ni kigeugeu kwa kuwa mwezi mmoja tu uliopita alitamka kuwa kama CCM ingempitisha Lowassa angehama chama hicho na kupinga uamuzi huo lakini leo ndiye anayempigia debe.

Aliikosoa vikali hotuba ya Edward Lowassa ya kuwatoa gerezani Babu Seya na mwanae wanaotumikia kifungo jela kwa kosa la kuwalawiti watoto wadogo.

Hakusita kuonesha uchungu aliokuwa nao kwa jinsi alivyoshiriki kwa nguvu yeye na mkewe Josephine katika kukijenga chama hicho lakini kimegeuka na kuwakaribisha wageni hao aliwaita makapi.

Dk. Slaa alihitimisha kwa kutangaza rasmi kustaafu siasa za vyama na kueleza kuwa ataendelea kushiriki katika harakati za kulikomboa taifa bila kujihusisha na chama chochote cha siasa huku akimtaka Lowassa kujitokeza hadharani kujibu alichokisema na kwamba akifanya hivyo atamrudia tena na mengine ambayo hajayatoa hadharani.

 

 

 

 

 

Gwajima Amjibu Dk. Slaa
Djilobodji Kuongeza Nguvu Chelsea