Kamati ya Kitaifa ya Maadili, Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini, imewaonya wanasiasa na makundi mbalimbali, kuacha mara moja kupotosha ukweli kuhusu nia njema ya rais Magufuli ya kupambana na kudhibiti usafirishaji wa mchanga wa dhahabu kwenda nje ya nchi.

Kamati hiyo pia imeitaka taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU), kuwabainisha wahusika wote, hususani vigogo wanaohusika na biashara hiyo ya usafirishaji mchanga nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Askofu, William Mwamalanga Jijini Dar es salaam, amesema kuwa Kamati imepokea suala hilo kwa masikitiko makubwa na kwamba huo ni uporaji wa wazi wa rasilimali za taifa.

“Kamati inalaani pingamizi juu ya suala hili, tunamuomba Rais Dkt. Magufuli asiishie kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini tu, bali rungu lishuke kwa kila mmoja aliyehusika na anaehusika na biashara hii,”amesema Mwamalanga.

Aidha, amesema kuwa Kamati hiyo imefanya utafiti wa kutosha kwa nchi za Japan na China, ambako mchanga huo hupelekwa na kujiridhisha kwamba, asilimia kubwa unakuwa ni madini halisi.

Machi 23 mwaka huu, Rais Dkt. Magufuli alipiga marufuku usafirishwaji wa makontena 20 baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es salaam, baada ya kubainika kuwa yana mchanga wa dhahabu.

Hata hivyo, kufuatia sakata hilo Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, liliingilia kati kwa kuunda Kamati itakayopitia sheria za mikataba yote ya madini na biashara hiyo

Video: Ney wa Mitego amgusa JPM, Mwigulu: Aliyemtishia Nape bastola siyo Polisi
Magazeti ya Tanzania leo Machi 28, 2017