Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Rais ya Afrika Kusini, ziara hiyo ni kufuatia vurugu za chuki dhidi ya wageni, ambazo zimesababisha mvutano baina ya mataifa hayo mawili.
Siku za hivi karibuni maeneo ya jiji la kibiashara la Afrika Kusini, Johannesburg, yalikumbwa na vurugu zilisosababisha mauaji dhidi ya wageni, wengi wa walengwa wakiwa wafanyabiashara wa Nigeria na mali zao.
Vurugu hizo zilisababisha mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya makupuni ya Afrika Kusini nchini Nigeria na kufungwa kwa muda mfupi kwa ubalozi wa Afrika Kusini mjini Lagos.
Takribani watu 10 walipoteza maisha katika vurugu hizo, huku idadi kubwa ya maduka yakiripotiwa kuharibiwa vibaya.
Hivyo, ziara ya Buhari ina lenga kuimarisha uhusiano baina ya mataifa hayo mawili na kufanya jitihada ya pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili watu na biashara kati ya Afrika Kusini na Nigeria.