Wanajeshi wanne wa Tunisia wamefariki wakati helikopta ya kijeshi waliyokuwa wakisafiria kuanguka baharini kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, huku Rais Kais Saied akisisitiza umuhimu wa kukarabati vifaa vya kijeshi.
Akitoa rambirambi zake kwa familia zilizofiwa, rais huyo alisema katika mkutano na Waziri wa Ulinzi Imed Memmiche kwamba ajali hiyo ilisababisha vifo vya wanajeshi wanne, ambapo awali Wizara ya Ulinzi iliarifu kuhusu miili miwili iliyopatikana baharini.
Wizara hiyo imesema mawasiliano yalipotea na helikopta ambayo ilikuwa ikifanya safari ya usiku katika mji wa Cape Serrat siku ya Jumatano jioni ikiwa na wafanyakazi wane ndani ya ndege.
Jeshi la Tunisia limepoteza ndege kadhaa katika mafunzo au operesheni za uchunguzi katika miaka ya hivi karibuni ambazo zilianguka ama kupata ajali.