Baada ya mjadala wa miaka mitatu, wananchi wa Chile sasa ni rasmi wameikataa katiba mpya ambayo ingehalalisha mambo mbalimbali ambayo mengine yangeweza kuwa na nafuu na baadhi yakiwa na ukakasi.
Mambo hayo ni pamoja na utoaji wa mimba, kuagiza huduma ya afya kwa wote, kuhitaji usawa wa kijinsia serikalini, kuyapa makundi ya watu asilia uhuru zaidi, kuviwezesha vyama vya wafanyakazi, kuimarisha kanuni za uchimbaji madini na kutoa haki kwa viumbe na wanyama.
Hatua hiyo, inafanya hitimisho la mchakato mrefu wa mapinduzi ya kisiasa, ambapo katika kura ya 2020, karibu Wachile wanne kati ya watano walisema wanataka katiba mpya lakini maono ya mabadiliko yalionekana kuwa makubwa huku asilimia 72 ya kura zikihesabiwa na asilimia 62 ya Wachile wakikataa waraka huo.
Katiba hiyo mpya, ingeweka zaidi ya haki 100 katika katiba ya kitaifa ya Chile na kuwa zaidi ya nyingine yoyote duniani na sasa Taifa hilo limesalia na mfumo uleule wa sheria ambao una mizizi yake katika udikteta na ukatili wa Jenerali Augusto Pinochet, aliyetawala kuanzia 1973 hadi 1990.
Rais wa Chile wa mrengo wa kushoto, Gabriel Boric amesema wapiga kura wanapaswa kuchagua mkutano wa katiba mpya ili kuandaa pendekezo lingine na kuanza tena mchakato mpya.
Hata hivy, Boric anakabiliwa na mporomoka wa viwango vya kuidhinishwa, huku kukiwa na ongezeko la mfumuko wa bei na uhalifu ambapo matarajio yake ya katiba mpya kumwezesha kutekeleza maono ya mrengo wa kushoto kwa nchi yamekwama.