Umoja wa Wastaafu Tanzania REAT wameiomba Serikali kusogeza huduma karibu za uhakiki na kubuni teknolojia itakayosaidia kukamilisha zoezi hilo badala ya kutumia mwendo na mda mrefu kufatilia uhakiki kwenye ofisi za NSSF na PSSF.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mikutano wa wanachama wa REAT mkoa wa Kagera mwenyekiti wa bodi ya wadhamini Gracian Mukoba ameeleza kuwa kuna haja ya serikali kutumia mfumo wa teknolojia kuwahakiki wazee badala ya wao kutumia muda na mwendo mrefu kufanya zoezi hilo.
Amesema, “Wastaafu kuja kuhakikiwa mkoani mstaafu anatoka sehemu inaitwa Bugarama iko Ngara karibu na Burundi huko anakuja mkoani kuhakikiwa kama bado yupo au alishaondoka kumbe jambo hili linaweza kufanyika kiteknolojia wakatumia simu wakawasiliana mpaka wakampata kwamba huyu mtu yupo zaidi ya kumsafirisha mwingine ana magongo anahitaji usaidizi, analipa nauli kwaajili ya jambo dogo.”
Aidha, ameongeza kuwa ” wastaafu wengi wana pensheni ndogo na hii ya mda mrefu haibadiliki, kwahiyo wito wa REAT ni kwamba serikali iangalie namna ya kuboresha pensheni za wastaafu ili na wenyewe waishi maisha ya furaha.”
Hata hivyo, katika kuhakikisha wastaafu wanatumia vyema mafao yao ya kustaafu Meneja wa tawi la benki ya Tanzania Commercial Bank – TCB tawi la Bukoba Samson Kayange amewasisitiza wastaafu hao kuwa makini dhidi ya matapeli wa mitandaoni.
Samson amesema “matapeli wanakuwa wengi kwa wastaafu kwasababu wanajua mna pesa, kwahiyo utakutana na watu wengi wanajifanya wanatoka kwenye mifuko, Afisa wa benki, mwekezaji ili tu akutapeli pesa ambayo unayo kwahiyo ni vizuri tukaepukana na matapeli, unashida benki njoo benki utuone usipigiwe na mtu.”