Watoto saba wameuawa nchini Niger katika shambulio la anga la jeshi la Nigeria likiwalenga “majambazi”.

Gavana wa eneo hilo Chaibou Aboubacar na vyombo vya habari vya serikali vimesema Watano wengine walijeruhiwa katika shambulio hilo linaloonekana kuwa lilifanywa kwa bahati mbaya katika kijiji cha Nachade.

Alisema wanne waliuawa papo hapo na watatu walifariki wakiwa njiani kupelekwa hospitalini.

Aboubacar alisema wazazi wa waathiriwa walikuwa wakihudhuria sherehe na “watoto hao yamkini walikuwa wakicheza” wakati mashambulizi ya anga yalipowakumba.

Alisema anaamini kuwa ndege hizo zilikuwa zikilenga “majambazi wenye silaha” katika maeneo ya mpaka kati ya nchi hizo mbili lakini zilikosa lengo na kugonga kijiji cha Nachade katika eneo la Madarounfa.

Niger na Nigeria zimekuwa zikiendesha operesheni za kijeshi za pamoja dhidi ya magenge yenye silaha yanayohusika na wimbi la utekaji nyara na mauaji katika eneo hilo.

Tangu mwaka 2018 Niger imeimarisha doria za kijeshi katika mpaka wake na Nigeria ili kuzuia uvamizi wa magenge hayo.

Vifo vya watoto hao vimekuja miezi mitatu tu baada ya watoto 26 wenye umri wa miaka mitano na sita kufariki katika ajali ya moto katika shule moja katika mji wa Maradi.

Maafisa wa Nigeria wamesema uchunguzi umeanza kuhusu tukio hilo.

Malkia Elizabeth aambukizwa virusi vya Corona
Mbasi ya umeme kutumia barabara za BRT