Naibu Waziri Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange amemsimamisha kazi Kaimu Mhandisi wa Wilaya ya Bunda, Timothy Mwajara na kuwata Mkurungenzi Changwa Mkwazo na Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo, Jamaly Kimamba kutathimini utendaji wao wa kazi kwa kushindwa kusimamia ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Bunda.
Dkt. Dugange ametoa maelekezo hayo hii leo Januari 13, 2023 wakati akikagua ujenzi wa hospitali ya wilaya Bunda na kutoridhishwa na kasi ya ujenzi na thamani ya fedha zilizotumika ambao mpaka sasa umeghalimu bilioni 3 na milioni 600.
Amesema, “Mhandisi wa Wilaya ya Bunda ana mwaka mmoja tangu ameletwa katika Halmashauri hiyo lakini ameshindwa kusimamia kikamilifu ujenzi wa majengo ya Hospitali hiyo na kamuagiza Katibu Tawala Mkoa kuleta Mhandisi mwingine atakaweza kusimamia ujenzi wa hospital hiyo.”
Dkt. Dugange amesema wakati akikagua hospitali hiyo ameona kuna vifaa ambavyo vimenunuliwa tangu mwaka 2019, ikiwemo madirisha ya aluminium, milango, vigae na mbao lakini hayajafungwa katika maeno yake na kupekea kuharibika na vingine kuibiwa.
Aidha, Dkt. Dugange amesema tangu mwezi wa tano mwaka 2019 Serikali ilitoa bilioni 1 na milioni 800 kujenga majengo saba ya awali lakini mpaka sasa hayajakamilika kwa sababu Watendaji waliosimamia ujenzi walifanya ubadhilifu wa fedha na walishindwa kusimamia.
Ameagiza kupatiwa majina watumishi wote ambao walihusika katika usimamizi wa ujenzi wa hospitali hiyo ambao wamehamishiwa maeno mengine ikiwa ni pamoja Waganga wakuu, Wahandisi, Maafisa manunuzi wa watumishi wengine ili waweze kurudi kujibu tuhuma na kuchukuliwa hatua stahiki.
Dkt. Dugange pia ameagiza Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwa kushirikiana na TAKUKURU kuchunguza thamani ya fedha iliyotumika kama inaendana na kazi iliyofanyika mpaka sasa na tuhuma mbalimbali ikiwa ni pamoja na wizi ambao umekuwa ukifanyika mara kwa mara ili wahusika wote waweze kuchukuliwa hatua sitahiki.