Zikiwa zimebaki siku chache kuukaribisha mwaka mpya wa 2017, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameeleza kuridhishwa na uhusiano wa kikazi kati ya vyombo vya habari na Serikali inayoongozwa na Rais John Magufuli, kwa kipindi cha mwaka mmoja uliokamilika.

Akizungumza jana Mkoani Lindi, Waziri Mkuu alisema kuwa anavipongeza vyombo vyote vya habari kwa kazi kubwa walioifanya ya kuueleza umma kazi iliyofanywa na Serikali pamoja na kuieleza Serikali maoni mbalimbali ya wananchi.

“Nichukue nafasi hii kupongeza vyombo vya habari vyote nchini kwa kazi nzuri mliyoifanya. Kwa ushirikiano mzuri mlioutoa kwa Serikali yetu, kwa kipindi cha mwaka mmoja ambao Mheshimiwa Rais ameendelea kutuongoza huku tukifanya kazi pamoja na vyombo vya habari,” alisema.

“Tumeshuhudia mawaziri mbalimbali wakiandamana na waandishi wa habari kwenye ziara zao kueleza kazi wanazokwenda kuzifanya. Na tumeshuhudiwa wananchi mbalimbali wakitumia vyombo vya habari kueleza tatizo lililoko mahali, na tumeona viongozi wa Serikali wakikimbia mara moja,” aliongeza.

Waziri Mkuu yuko Mkoani Lindi kwa ziara itakayogusa wilaya zote za mkoa huo, na amezitaka wilaya zote za mkoa huo kujifunza namna Wilaya ya Liwale ilivyofanikiwa katika jitihada za kuboresha elimu na kufanikiwa kushika nafasi ya kwanza kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo.

Waziri Mkuu pia aliibana Bodi ya Korosho mkoani humo akitaka ieleze sababu zinazopelekea malipo ya wakulima kucheleweshwa, kinyume na maagizo ya Serikali.

BoT yadaiwa shilingi 3.5 bilioni
Tanzania yachunguza madai ya Malawi kuwakamata wapelelezi wake