Usaliti wa mapenzi unatajwa kuwa moja kati ya vyanzo vikuu vitatu vinavyosababisha vita na migogoro mikubwa katika jamii na hata kuwafanya watu waape kutozikana.

Hili limethihirishwa hivi karibuni pia kuwa chanzo cha kulivunja kundi maarufu la Rap nchini, Mexicana Lacavela lililovuma miaka michache iliyopita.

Kiongozi wa kundi hilo, Baghdad ambaye hivi sasa anafanya kazi kama msanii wa kujitegemea alikiambia kipindi cha The Playlist cha 100.5 Times Fm kuwa usaliti wa mapenzi kati yao ndio chanzo kikuu kilichovunja kundi na kuleta uhasama wa kudumu kati yake na mtayarishaji wa muziki aliyekuwa mwana-Mexicana, Mensen Selekta.

Rapa huyo alieleza kuwa Mensen alimgeuka na kumchukua mpenzi wake aliyemtaja kwa jina la ‘Anita’, ambaye anaonekana kwenye video ya wimbo wa ‘Tilatila’ wa Mr. Blu. Alieleza kuwa aligundua rafiki yake huyo wa karibu anakula tunda lake na kuamua kufuatilia, ndipo alipokutana na ukweli uso kwa macho uliomuumpasua kichwa.

“Nilisikia siku moja wameenda kwenye hotel fulani wamechukua chumba, na hiyo ni baada ya Anita kuniomba kiasi cha zaidi ya shilingi 200,000. Nilimpa kama alivyoniomba. Nilipofika kwenye hotel nikaangalia kwenye daftari la wageni nikakuta ile ‘From Dar… To Dar’, majina yakaeleza kila kitu. Niliumia sana,” alisimulia.

Baghdad anasema kilichomuuma zaidi ni pesa aliyompa mwanamke huyo ambayo anahisi ilitumika kufanikisha tukio la kumsaliti.

Baada ya tukio hilo, Baghdad alijitoa kundini. Na kwa kuwa alikuwa kiungo muhimu hususan upande wa promotion, alikataa kupokea kazi yoyote ya msanii wa kundi hilo inayotoka kwa Mensen na kufunga mirija ya kutokea, huku Mensen pia akizuia upande wake. Hivyo, Mexicana ambayo wakati huo ilikuwa inatamba na wimbo wa ‘Kamba To Kamba’ ikichuana vikali na Kundi la Lunduno, ikafikia tamati.

Hata hivyo, uhasama kati ya wawili hao haujaisha, na hadi sasa Baghdad anasema amemsamehe Mensen lakini hataweza kuwa rafiki yake milele.

Hivi sasa, Baghdad ambaye ni mwanandoa, ameachia Documentary yake aliyoipa jina la Since 92.

 

Baghdad na Mkewe wa ndoa

Baghdad na Mkewe wa ndoa

Mexicana ilikuwa inaundwa na wasanii wenye vipaji wakiwemo Bagdad, Tana, Chibwa na wengine.

 

Serikali yawanyooshea kidole wanaofungisha ndoa
Sakata la Zanzibar lamponza Lissu, Ahojiwa na Polisi saa nzima