Klabu ya Zamalek SC ya MIsri imethibitisha kuwa mshambuliaji wao nyota, Mostafa Mohamed yuko katika hatua nzuri za kujiunga na miamba ya jiji la Istanbul, Galatasaray ya Uturuki kwa mkopo.

Mohamed amekuwa akihusishwa na taarifa zakuondoka Zamalek kwa muda sasa, na timu kadhaa za Barani Ulaya zimekua zikionesha nia ya kutaka kumsajili mshambuliaji huyo, ambaye pia ana umuhimu mkubwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Misri.

Mchezaji huyo wa miaka 23 alikaribia kujiunga na klabu ya Saint-Étienne inayoshiriki Ligi ya Ufaransa (Ligue 1), lakini kuvunjikwa kwa mazungumzo baina ya viongozi wa pande hizo mbili, kulifanya dili hilo kuingia gizani.

Saint-Étienne waliripotiwa kutuma ofa ya Dola za Kmarekani milioni 5 kwa Zamalek, ili kufanikisha kuipata huduma ya Mostafa Mohamed lakni ilikataliwa.

Klabu ya Galatasaray ya Uturuki ilitumia nafasi hiyo kwa kuanzisha mazungumzo na viongozi wa Zamalek, na taarifa zinaeleza kuwa Mohamed anatarajiwa kuwasili nchini Uturuki mwishoni mwa juma hili kukamilisha taratibu za uhamisho wake.

Hata hivyo atajiunga na Galatasaray kwa mkopo wa mwaka mmoja na nusu, lakini atakua na nafasi ya kusajiliwa moja kwa moja endapo ataonesha kiwango cha kuridhisha.

Ada ya usajili wa mkopo kwa mshambuliaji huyo inatajwa kufikia Dola za Kimarekani milioni 2, na Ikiwa wataamua kumsajili moja kwa moja, Galatasaray watalazimika kulipa ada ya Dola za Kimarekani milioni 4.

Mohamed anaweza kuchukua nafasi ya Mbaye Diagne wa Senegal, ambaye inasemekana yuko tayari kukamilisha uhamisho wa kwenda West Brom ya England kwa mkopo.

Diagne alikuwa amefunga mabao tisa katika michezo 15 aliyochezea Galatasaray kwenye Super Lig ya Uturuki msimu huu.

Bumbuli: Nililipa faini na pay slip nilipeleka TFF
Majaliwa ataka wamachinga wakumbukwe