Wafanyakazi 597 walioachishwa kazi na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) hivi karibuni, wameandamana hadi katika ofisi za Mamlaka hiyo zilizoko Victoria jijini Dar es Salaam wakidai stahiki zao.

Wafanyakazi hao ambao mikataba yao ya kazi imevunjwa ghafla kutoka na kile kilichoelezwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka, Dk Modestus Kipilimbahiyo kuwa ni ufinyu wa bajeti, wameeleza kuwa wanadai malimbikizo ya mishahara yao ya miezi mitatu.

Wameeleza kuwa uamuzi wa serikali kusitisha mikataba yao bila kuwapa ‘notice’ haikuwa sahihi na ni kinyume cha sheria ya Kazi.

“Wameamua kuturudisha nyumba lakini wanatakiwa kutulipa stahiki zetu na mishahara ya miezi mitatu,” alisema Seif Kibangu, kiongozi wa wafanyakazi hao.

Aliongeza kuwa baada ya kusikia kupitia vyombo vya habari kuwa mikataba yao imesimamishwa walienda kuangalia masalio yao kwenye mfuko wa jamii wa GEPF na kubaini kuwa Mamlaka hiyo ilikuwa haijawawalipia michango yao tangu Julai mwaka jana.

Aidha, aliyekuwa Mtaalamu wa takwimu, Joseph Mtitu alieleza kushangazwa na taarifa hizo za kusimamishwa kwao akidai kuwa walizisikia kwenye vyombo vya habari kabla ya muajiri hajawataarifu.

Wakizungumzia sababu za ufinyu wa bajeti na kutokuwa na ufanisi kazini, zilizotolewa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, wafanyakazi hao walisema kuwa suala la kutokuwepo kwa ufanisi lilisababishwa kutokuwepo kwa rasilimali za kutosha pamoja na vitendea kazi.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo alikiri kuwepo kwa upungufu wa vitendea kazi visivyoendana na idadi ya wafanyakazi pamoja na ufinyu wa bajeti uliopelekea kutolipa mishahara yao kwa miezi mitatu, hali inayoweza kuchangia kutokuwepo kwa ufanisi.

 “Ni kweli kwamba wafanyakazi hao hawakulipwa mishahara yao ya miezi mitatu kwa sababu hakuna fedha. Nitahakikisha wanalipwa fedha hizo lakini kwa sasa hakuna kazi. Hebu fikiria, tuna kompyuta 150 tu wakati wafanyakazi hao wako 597, hatuwezi kwenda,” alisema Dk. Kipilimba.
Watumishi hao wanadai jumla ya shilingi milioni 900.

 

 

 

 

 

 

Wajumbe Wa TFF Kukutana Mwishoni Mwa Juma Hili
Tata Martino Atangaza Kikosi Cha Argentina